59. Uombezi wa pili, tatu na nne ambao ni wa Mtume

2- Uombezi wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya watu wa Peponi waingie ndani na wafunguliwe. Yeye ndiye wa kwanza atayefunguliwa mlango wa Peponi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hii amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا

“Na wataendeshwa wale waliomcha Mola wao kuelekea Peponi hali ya kuwa makundimakundi, mpaka watakapoifikia na ikafunguliwa milango yake.”[1]

Si kwamba mara tu watapofika watafunguliwa. Ameegemeza ufunguzi juu ya ujio kwa sababu watafunguliwa baada ya kufanyiwa uombezi

وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِّنكُمْ يَتْلُونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِ رَبِّكُمْ وَيُنذِرُونَكُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا ۚ قَالُوا بَلَىٰ وَلَـٰكِنْ حَقَّتْ كَلِمَةُ الْعَذَابِ عَلَى الْكَافِرِينَ قِيلَ ادْخُلُوا أَبْوَابَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۖ فَبِئْسَ مَثْوَى الْمُتَكَبِّرِينَ وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ

“… na walinzi wake watawaambia: “Je, hawakukujieni Mitume katika nyinyi, wakikusomeeni Aayah za Mola wenu na wakikuonyeni kukutana na siku yenu hii? Watasema: “Ndio bila shaka!” Lakini neno la adhabu limehakiki juu ya makafiri. Itasemwa: “Ingieni milango Motoni hali ya kuwa ni wenye kudumu humo. Basi ubaya ulioje makazi ya wanaofanya kiburi! Na wataendeshwa wale waliomcha Mola wao kuelekea Peponi hali ya kuwa makundimakundi, mpaka watakapoifikia na ikafunguliwa milango yake, na watasema walinzi wake: “Amani iwe juu yenu furahini na ingieni hali ya kuwa ni wenye kudumu.”[2]

Kuhusu makafiri mara tu watapofika Motoni itafunguliwa milango yake, watasukumwa na kuvurumishwa ndani yake kwa nguvu:

وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا فُتِحَتْ أَبْوَابُهَا

“Wataendeshwa wale waliokufuru kuelekea Motoni wakiwa makundimakundi, mpaka watakapoufikia, itafunguliwa milango yake.”[3]

Huu ni uombezi wa pili wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ni maalum kwake.

3- Atawaombea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) watu katika watu wa Peponi ili zinyanyuliwe ngazi zao Peponi.

4- Uombezi wake juu ya ami yake Abu Twaalib. Uombezi hauwafai kitu makafiri. Lakini kwa kuzingatia kwamba Abu Twaalib alimhami, kumtetea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akasubiri pamoja naye katika dhiki na akamtendea wema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini pamoja na hivyo hakujaaliwa kuingia ndani ya Uislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuonyesha Uislamu na akapupia aingie ndani ya Uislamu. Lakini hata hivyo akakataa kwa sababu alikuwa anaona kuingia ndani ya Uislamu ni kutukana dini ya babu zake. Alishikwa na mori za kijaahiliyyah juu ya dini za babu zake. Vinginevyo anatambua kuwa Muhammad yuko katika haki na kwamba dini yake ndio ya haki. Lakini kasumba na majivuno ndio vilivyomzuia. Kwa sababu alikuwa anaona kwa madai yake akisilimu basi itakuwa ni matusi kwa kabila lake. Yeye ndiye aliyesema:

Nimejua kuwa dini ya Muhammad

ni miongoni mwa dini za viumbe bora kabisa

Laiti kama si lawama au kuchelea matusi

Mgeniona ni mwenye kujisalimisha kwayo[4]

Lawama na kuchelea watu wake wasije kumtukana ndivo vilivyomzuia. Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimjia akiwa katika hali ya kukata roho. Akamwambia:

“Ee ami yangu! Sema “Laa ilaaha illa Allaah”. Ni neno nitalokutetea kwalo mbele ya Allaah.”

Mbele yake alikuwa Abu Jahl na ´Abdullaah bin Umayyah ambao wakamwambia: “Hivi kweli unataka kuiacha dini ya ´Abdul-Muttwalib?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamrudilia nao wakamrudilia na kumwambia: “Hivi kweli unataka kuiacha dini ya ´Abdul-Muttwalib?” Akasema kwamba yeye yuko katika dini ya ´Abdul-Muttwalib na akafa juu ya hilo na akakataa kutamka shahaadah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Nitakuombea msamaha midhali sijakatazwa.”[5]

Ndipo Allaah akateremsha maneno Yake (Ta´ala):

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُمْ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ

“Haimpasi Nabii na wale walioamini kuwaombea msamaha washirikina japokuwa ni jamaa zao wa karibu baada ya kuwabainikia kwamba wao ni watu wa Motoni.”[6]

Akateremsha juu ya Abu Twaalib:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ

”Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendaye, lakini Allaah humwongoza amtakaye; Naye ndiye mjuzi zaidi ya waongokao.”[7]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawezi kuombea juu ya kumtoa Motoni. Kwa sababu atadumishwa Motoni milele. Lakini atamuombea afanyiwe wepesi adhabu peke yake. Atawekwa juujuu kwenye Moto na chini ya nyayo zake za miguu atawekewa makaa mawili yatayochemsha ubongo wake. Ataona kuwa hakuna mwenye adhabu kali kama yeye pamoja na kuwa yeye ndiye mwenye adhabu nyepesi katika watu wa Motoni[8]. Huu ni uombezi maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 39:73

[2] 39:72-73

[3] 39:71

[4] Tazama ”al-Bidaayah wan-Nihaayah” (03/42) ya Ibn Kathiyr na ”al-Iswaabah” (07/236) ya Ibn Hajar.

[5] al-Bukhaariy (1360) na Muslim (24) kupitia kwa Sa´iyd bin Musayyib kutoka kwa baba yake.

[6] 09:113

[7] 28:56

[8] Tazama ”Swahiyh-ul-Bukhaariy” (3883) na ”Swahiyh-ul-Muslim” (209).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 86-87
  • Imechapishwa: 09/04/2021