57. Kugamegawanyika kwa watu mafungu matatu juu ya suala la uombezi


Suala la uombezi watu wamegawanyika mafungu matatu:

La kwanza: Wale ambao wamepinga uombezi. Ni Khawaarij na Mu´tazilah. Wamesema kuwa mwenye kustahiki Moto ni lazima aingie ndani. Hayo ni kutokana na imani yao kwamba makafiri ndio wenye kustahiki Moto. Kwa sababu wanawakufurisha waislamu wenye kutenda madhambi makubwa. Kwa hiyo wanaona kuwa hautomfaa kitu uombezi. Yule mwenye kustahiki Moto ni lazima aingie ndani na mwenye kuingia ndani hatotoka nje. Haya ndio madhehebu yao.  Kwa hivyo wanapinga uombezi uliyothibiti na kupokelewa kwa dalili nyingi.

La pili: Wale ambao wamechupa mpaka katika kuthibitisha uombezi. Nao ni waabudia makaburi na makhurafi ambao wanawategemea wafu, wanawaomba uombezi, wanawaabudia, wanawachinjia na wanawawekea nadhiri. Wakiambiwa kwamba matendo hayo ni shirki wanasema kuwa ni kuomba uombezi. Ni kama walivosema washirikina wa kale:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[1]

Wamechupa mpaka katika kuthibitisha uombezi mpaka wakafikia kuuomba kwa asiyekuwa Allaah. Wameuomba kutoka kwa wafu, kutoka kwa waliyomo ndani ya makaburi na kutoka kwa wasiostahiki ambao ni washirikina na wenye kumkufuru Allaah (´Azza wa Jall).

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ndio waliofanya kati na kati, kama ilivyo kawaida yao. Ni wenye kufanya kati na kati katika mambo yote. Hawakupinga uombezi moja kwa moja, kama walivyofanya Khawaarij na Mu´tazilah na hawakuuthibitisha moja kwa moja, kama walivyofanya waabudia makaburi na makhurafi. Haya ndio madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya masuala haya. Miongoni mwa mambo yatayopitika siku ya Qiyaamah ni pamoja na uombezi. Kwa ajili hiyo ndio maana mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amelitaja katika jumla ya mambo yatayokuwa siku ya Qiyaamah; kwamba mtu anatakiwa kuamini yale yote yatayokuwa siku ya Qiyaamah kukiwemo uombezi.

[1] 10:18

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 09/04/2021