2- Aliyekufa shahidi. Kumepokelewa Hadiyth nyingi juu ya hilo. Nitatosheka kutaja baadhi yake:

Ya kwanza: Shaddaad bin al-Haadiy ameeleza:

“Kuna bwana mmoja katika mabedui alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akamwamini na akamfuata. Kisha akasema: “Nahajiri pamoja nawe.”… Wakakaa kitambo kidogo. Kisha wakaandoka kumpiga vita adui. Baadaye wakamleta kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakiwa wamembeba na mshale umempiga pale alipoashiria… Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamvika sanda ndani ya joho la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamtanguliza mbele na kumswalia… “

Ameipokea an-Nasaa´iy na wengineo kwa cheni ya wapokezi nzuri. Imekwishatangulia kwa utimilifu wake katika masuala ya 39, ukurasa wa 61.

Ya pili: ´Abdullaah bin az-Zubayr amesema:

“Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamrisha Hamzah siku ya Uhud avikwe sanda kwenye shuka lenye michirizimichirizi kisha akamswalia ambapo akaleta Takbiyr mara tisa, kisha akaletewa wafu waliowawa hali ya kuwa wamepangwa safu ambapo akawaswalia na yeye (Hamzah akamswalia tena) pamoja nao.”

Ameipokea at-Twahaawiy katika “Maaniy al-Aathaar” (01/290) kwa cheni ya wapokezi nzuri. Wapokezi wake wote ni waaminifu na wenye kutambulika. Abul-Ishaaq amezungumza kwa kuweka wazi.

Pia ina shawahidi nyingi. Nimetaja baadhi yake katika “at-Ta´liyqaat al-Jiyaad” katika masuala ya 75.

Ya tatu: Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Hakka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpitia Hamzah bin ´Abdil-Muttwalib ilihali amenyofolewanyofolewa na amekatwakatwa viungo na wala hakumswalia yeyote katika mashahidi isipokuwa yeye tu. Bi maana mashahidi wa Uhud[1].”

Ameipokea Abu Daawuud kwa cheni ya wapokezi nzuri. Ni mukhtasari wa Hadiyth iliotangulia katika masuala ya 37, ukurasa wa 57-58.

Ya nne: ´Uqbah bin ´Aamir al-Juhaniy  ameeleza:

“Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka siku moja akamswalia mfano wa swalah yake kumswalia maiti [baada ya kupita miaka nane] [kana kwamba anawaaga waliohai na waliokufa] kisha akaenda kwenye mimbari yake [akamhimidi Allaah na kumsifu] akasema: “Mimi ni mwenye kukutangulieni na mimi ndiye nitayekushuhudieni [hakika miadi yenu na mimi ni hodhi] naapa kwa  Allaah kwamba ni mwenye kuiona hodhi hivi sasa [na hakika upana wake ni kama baina ya Iylah mpaka Juhfah]. Hakika mimi nimepewa funguo za mali za hazina za ardhini au funguo za ardhi. Naapa kwa Allaah kwamba mimi sichelei juu yenu kwamba mtafanya shirki baada yangu, lakini ninachochelea juu yenu [ni dunia] mkaja kushindana juu yake [na mkauwana ambapo mkaangamia kama walivyoangamia waliokuwa kabla yenu. Msimulizi anaeleza: “Hilo ndio lilikuwa jicho la mwisho kumuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”]

Ameipokea al-Bukhaariy (03/164-07/279-280 na 302), Muslim (07/67), Ahmad (04/149, 153, 154) na mtiririko ni wa al-Bukhaariy. Ziada ya kwanza, ya pili, ya sita na ya saba ni yake. Muslim anayo pia ziada ya pili, ya tano na zilizo nyuma yake. Ahmad pia anayo ziada ya kwanza mpaka ya nne. Ameipokea pia al-Bayhaqiy (04/14) na kwake ziko ziada zote isipokuwa ya tatu na ya tano. Ameipokea pia at-Twahaawiy (01/290), an-Nasaa´iy (01/277), ad-Daaraqutwniy (uk. 197) kwa mukhtasari. Kwa ad-Daaraqutwniy ipo ziada ya kwanza.

Huenda akasema mwenye kusema: “Imethibiti kupitia Hadiyth hizi kwamba ni jambo limewekwa katika Shari´ah kuwaswalia mashahidi na msingi ni kwamba ni wajibu. Ni kwa nini basi mtu asisemi kuwa ni wajibu?” Ni kutokana na yale tuliyotangulia kutaja katika masuala ya 58. Tunaongeza juu ya hayo kwa kusema:

“Wako Maswahabah wengi katika Badr na kwenginepo waliokufa shahidi. Haikunakiliwi kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalia. Lau ingefanya hivo basi tungenukuliwa kutoka kwake. Hivyo imejulisha kwamba kuwaswalia sio kitu cha lazima. Ndio maana Ibn-ul-Qayyim amesema katika “Tahdhib-us-Sunan” (04/295):

“Maoni ya sawa ni kwamba mtu ana khiyari kati ya kuwaswalia na kuacha kufanya hivo. Hilo ni kutokana na kupokelewa mapokezi kwa yote mawili. Kumepokelewa moja ya mapokezi kutoka kwa Imaam Ahmad na inayoendana na misingi na madhehebu yake.”

Hapana shaka kwamba kuwaswalia ndio bora zaidi kuliko kuwaacha kukiwepesika kufanya hivo. Kwa sababu ni du´aa na pia ni ´ibaadah.

[1] Pengine anachokusudia ni kumswalia mwengine akiwa peke yake. Haitakikani kuwaswalia wengine wakiwa wameambatanishwa naye, kama ilivyo katika Hadiyth ilio kabla yake. Hadiyth hizi mbili hazipingani na Hadiyth ya Jaabir iliotangulia kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwaswalia mashahidi wa Uhud. Kwa sababu Hadiyth hiyo imekuja kukanusha. Anayethibitisha anatangulizwa mbele ya anayekanusha. Tazama upambanuzi zaidi katika “Nayl al-Awtwaar”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 104-108
  • Imechapishwa: 16/07/2020