59- Imependekezwa kuwaswalia wale ambao kunakuja utajo wao:

1- Mtoto ijapo ni kipomoko. Ni yule ambaye ameporomoka kutoka tumboni mwa mama yake kabla ya kutimiza siku zake. Kumepokelewa Hadiyth mbili juu ya hilo:

Ya kwanza: “… mtoto [Imekuja katika upokezi mwingine: “Kipomoko kinaswaliwa. Wazazi wake wataombewa msamaha na rehema.”

Ameipokea Abu Daawuud, an-Nasaa´iy na wengineo kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Imekwishatangulia kwa ukamilifu wake katika masuala ya 50.

Ya pili: “´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mtoto miongoni mwa watoto wa Answaar aliletwa mbele ya Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akamswalia. ´Aaishah akasema: “Twuubaa kwa mtoto huyu. Kidege miongoni mwa videge vya Peponi. Hajawahi kuona ovu lolote na wala kuyaona.” Akasema: “Au kuna jengine, ee ´Aaishah? Allaah ameiumba Pepo, akawaumbia wakazi wake, akawaumba na akawaumba wakiwa bado wako kwenye migongo ya baba zao. Pia ameumba Moto, akawaumbia wakazi wake, akawaumba na akawaumba wakiwa bado wako kwenye migongo ya baba zao.”

Ameipokea Muslim (08/55), an-Nasaa´iy (01/272), Ahmad (06/208) na tamko ni la an-Nasaa´iy. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Wapokezi wake wote ni waaminifu ni wapokezi wa Muslim mbali na mwalimu wake ambaye ni ´Amr bin al-Mansuur ambaye pia ni mwaminifu na imara.

an-Nawawiy amesema:

“Wanachuoni wa waislamu wanaotegemewa wameafikiana kwamba mwenye kufa katika watoto wa waislamu basi yuko Peponi. Jawabu juu ya Hadiyth hii ni kwamba pengine inakataza mtu kufanya haraka ya kukata moja kwa moja pasi na dalili au alisema hivo kabla ya yeye kujua kwamba watoto wa waislamu wako peponi.”

as-Sindiy amejibu katika maelezo yake ya chini juu ya “an-Nasaa´iy” kwa jibu jengine ambalo mukhtasari wake ni ifuatavyo:

“Kilichokatazwa ni mtu kumkatia moja kwa moja Pepo mtoto maalum. Wala haitosihi kukata kauli kwa mtoto maalum. Kwa sababu imani ya wazazi wake wawili kule kuihakiki kwake ni jambo la ghaibu. Isitoshe imani yao ni kitu tegemezi kwa Allaah (Ta´ala).”

Udhahiri ni kwamba kipomoko kinaswaliwa pale ambapo tayari kimeshapuliziwa roho. Hapo inakuwa pale ambapo ameshakamilisha miezi mine kisha akafa. Haswaliwi akifa kabla ya hapo kwa sababu kipomoko hicho sio maiti kama ambavo inatambulika. Msingi wa jambo hilo ni Hadiyth ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika kila mmoja wenu linakusanywa umbile lake tumboni mwa mama yake kwa masiku arubaini. Kisha inakuwa kipande cha damu kwa muda kama huo. Halafu inakuwa kinofu cha nyama kwa muda kama huo. Halafu anatumiwa Malaika kumpulizia roho…. ”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Baadhi ya wengine wameweka sharti kwamba kipomoke baada ya kwamba kilikuwa hai. Hilo ni kutokana na Hadiyth isemayo:

“Pindi kitaporomoka kitoto hali ya kupiga makelele basi kitaswaliwa na kurithiwa.”

Lakini ni Hadiyth dhaifu isiyojengewa hoja. Hivo ndivo walivyobainisha wanachuoni[1].

[1] Tazama ”Naswb-ur-Raayah” (02/277), ”at-Talkhiysw” (05/146-147), ”al-Majmuu´” (05/255) na kitabu  changu “Naqd-ut-Taaj al-Jaamiy´ lil-Usuwl-il-Khamsah” nambari (293). Hadiyth imesihi bila ya kutaja jambo la kukiswalia. Hayo nimeyahakiki katika “al-Irwaa´-ul-Ghaliyl” (1704) – Allaah afanye wepesi kukichapisha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 104-106
  • Imechapishwa: 16/07/2020