Mfungaji anatakiwa kujiepusha pia na uvumi. Nako ni kule kuyahamisha maneno kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa lengo la kuharibu kati yao. Ni dhambi kubwa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Hatoingia Peponi mmbea.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea tena kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita pambizoni na makaburi mawili ambapo akasema:

“Hakika wawili hawa wanaadhibiwa na wala hawaadhibiwi kwa jambo kubwa.”

Bi maana kwa kitu kigumu kwao.

“Ama mmoja wao alikuwa hajisafishi hajichungi na mkojo. Ama mwengine alikuwa akieneza uvumi.”

Uvumi unamuharibu mtu mmojammoja na jamii nzima, kufarikisha kati ya waislamu na kuingiza uadui kati yao:

وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ هَمَّازٍ مَّشَّاءٍ بِنَمِيمٍ

“Na wala usimtii kila mwingi wa kuapa, wa kutwezwa. Mwingi wa kukashifu, mwenye kueneza umbea.”[1]

 Jichunge na mmbea!

[1] 68:10-11

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 71
  • Imechapishwa: 22/04/2021