57. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu mipango na makadirio

Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

وبالقدرِ المقدورِ أيقِن فإنَّه

28 – Yakinisha makadirio yaliyopangwa, kwani hakika

دعامةُ عقدِ الدِّين والدِّينُ أفيحُ

     ndio nguzo ya dini na dini ni pana

MAELEZO

Kuamini makadirio ni nguzo ya sita miongoni mwa nguzo za imani. Jibriyl (´alayhis-Salaam) alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza amkhabarishe juu ya imani ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Imani kumuamini Allaah, Malaika Wake, vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na kuamini makadirio ya kheri na shari yake.”[1]

Akafanya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuamini makadirio ni nguzo ya sita ya imani.

Kuamini mipango na makadirio ni kule kuamini elimu ya Allaah (Jalla wa ´Alaa), kuyakadiria Kwake mambo kabla ya kutokea Kwake, matendo ya Allaah (Jalla wa ´Alaa), utashi na matakwa Yake na kuumba Kwake. Ni jambo tukufu. Katika Qur-aan amesema (Ta´ala):

وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا

“Ameumba kila kitu na Akakikadiria kipimo sawasawa.” (25:02)

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

“Hakika Tumekiumba kila kitu kwa makadirio.” (54:49)

Bi maana amekadiria kutokea kwake, kupatikana kwake na akayaumba. Vilevile akakadiria sifa na wakati wake ambapo yatatokea. Hivyo kila kitu kimekadiriwa kwa njia zake zote:

1 – Kwa njia ya kuyatambua.

2 – Kwa njia ya kuyaandika katika Ubao uliohifadhiwa.

3 – Kwa njia ya Allaah kuyataka kwa muda wake.

4 – Kwa njia ya kuyaumba.

Kila kitu kina sifa zake ambazo Allaah amezijaalia. Kitu hicho hakizidi na wala hakipungui. Hiki ni kitu pia kimekadiriwa. Kwa mfano amesema (Ta´ala) kuhusu mvua:

وَمَا نُنَزِّلُهُ إِلَّا بِقَدَرٍ مَّعْلُومٍ

“Hatuiteremshi isipokuwa kwa kadiri maalumu.” (15:21)

Kile kiwango, pahali inapoteremka na wakati itapoteremka yote Allaah anayajua kwa njia zake zote. Hakuna kitu isipokuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) alikijua , akakiumba na akakikadiria. Hakikupatikana pasi na kuumbwa, bila ya kutangulia kukadiriwa, bila ya kuandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa na wala pasi na Allaah (Jalla wa ´Ala) kukitaka kwanza. Mambo yanayopitika ulimwenguni hayapitiki hovyohovyo. Bali mambo hayo yamedhibitiwa kwa Allaah kuyakadiria, kuyaumba na kuyataka kwa sifa ilizonazo. Hili ni jambo muhimu sana.

Kuna watu vigogo ambao hawaangalii Aayah za Qur-aan na Hadiyth za kinabii waliopotea katika mambo haya. Wao wanategemea akili na fikira zao. Hivyo matokeo yake wakachanganya mambo hali ya kutia aibu katika mipango na makadrio. Upande mwingine Allaah akawaongoza Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wakaiamini kwa njia ambayo Allaah ameitaka na ameiwajibisha juu ya waja Wake kwa mujibu wa dalili za Qur-aan na Sunnah. Hii ndio ada yao katika milango yote inayohusiana na ´Aqiydah.

[1] Muslim (01) na (08)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 133-134
  • Imechapishwa: 11/01/2024