58. Maana ya mipango na makadirio na ulazima wa kuyaamini

Utafiti juu ya mipango na makadirio ndani yake kuna mambo mengi:

1 – Ni kuhusu maana ya mipango na makadirio. Makadirio ni Allaah (Jalla wa ´Alaa) kuyakadiria, kuyataka na kuyaumba mambo katika wakati wake. Hii ndio maana ya makadirio. Mara nyingi kunaposemwa ´mipango` na ´makadirio` hakuna tofauti kati yake. Hata hivyo mipango imeenea zaidi kuliko makadirio. Kwa sababu wakati mwingine mipango inakuja ikiwa na maana ya makadirio. Wakati mwingine inakuja ikiwa na maana ya kwamba Allaah amevikadiria vitu na kuvipanga. Vilevile wakati mwingine inakuja ikiwa na maana ya kuwahukumu watu kati ya yale waliyotofautiana:

إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ

“Hakika Mola wako atahukumu baina yao siku ya Qiyaamah katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana nayo.” (45:17)

Kwa hivyo mipango imeeneza zaidi kuliko makadirio.

2 – Kuhusu kuamini mipango na makadirio. Kuamini mipango na makadirio ni wajibu na ni faradhi juu ya muumini. Kwa kuwa ni nguzo miongoni mwa nguzo za imani sita. Jengine ni kwa sababu ni kuamini uwezo wa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Kwa ajili hii ndio maana amesema:

“Makadirio ni uwezo wa Allaah. Mwenye kuyapinga basi amepinga uwezo wa Allaah (Jalla wa ´Alaa).”[1]

Katika baadhi ya ibara vilevile imekuja:

“Makadirio ni siri ya Allaah kwa viumbe Wake.”[2]

Haijuzu kutafiti mipango na makadirio mtu akavuka zile dalili zilizokuja katika Qur-aan na Sunnah na akachupa mipaka katika kupekua. Haya hatimaye yanapelekea katika upotevu na kuchanganyikiwa. Kwa sababu ni siri ya Allaah kwa waja Wake. Pindi utapochupa mipaka na kufanya utafiti hutofikia natija yoyote. Kwa kuwa utakuwa ni mwenye kutafiti jambo ambalo Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameliwaficha viumbe Wake. Inatosha kwako kuamini peke yake. Hakuna yeyote aliyejikakama akafikia natija yoyote. Bali kinyume chake alifikia katika kuchanganyikiwa. Kwa ajili hiyo inatosheleza kwako kutembea kwa mujibu wa dalili zilizothibiti katika Qur-aan na Sunnah juu ya kuthibitisha makadirio na kuiamini. Haya yanakutosheleza.

[1] Ibn Battwah katika “al-Ibaanah” (02/231) na “al-Minhaaj-us-Sunnah an-Nabawiyyah” (03/254)

[2] al-Laalakaa´iy katika “I´tiqaad Ahl-is-Sunnah” (1122) (03/1122) na Abu Na´iym katika “al-Hilyah” (06/181)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 134-136
  • Imechapishwa: 11/01/2024