Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Kuna mwingine tena katika wao amesema:

“Watu wenye shaka zaidi wakati wa kufa ni wanafalsafa.”

Isitoshe wanatheolojia hawa wanaoenda kinyume na kaguzi za Salaf, mtu ataona kuwa wanakosa ule ujuzi safi wa kumtambua Allaah.

MAELEZO

Huu ni ushahidi wa mwingine katika wao jinsi ambavyo mfumo wa wanafalsafa ni batili. Wao wenyewe wanaitilia shaka ´Aqiydah yao wakati wa kutaka kukata roho. Kwa sababu hawakuchukua kitu kinachowaokoa wakati wa kufa. Wanakuwa katika hali ya kuchaganyikiwa na vurugu mpaka zinapotolewa roho zao.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) bado anaendelea kubainisha tofauti kati ya ´Aqiydah ya Salaf katika majina na sifa za Allaah, na ´Aqiydah ya wale waliokuja nyuma. Hakika Salaf (Rahimahumu Allaah) wameichukua elimu yao kutoka katika Qur-aan na Sunnah – kutoka katika vyanzo viwili hivi vikubwa – kupitia kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanafunzi wa Maswahabah na vile vizazi bora. Kuhusu wale waliokuja nyuma hawana sifa hizi za kipekee. Wengi wao wameichukua elimu yao kutoka katika mijadala na mantiki; watu ambao wameijenga ´Aqiydah yao kutoka katika mijadala na mantiki. Ipo tofauti kubwa kati ya ambaye anaijenga ´Aqiydah yake kutoka katika Qur-aan, Sunnah n Salaf, na ambaye anaijenga ´Aqiydah yake kutoka kwa watu hawa ambao hawana utambuzi wowote juu ya Allaah na yale yanayolingana Naye. Wale waliokuja nyuma hawamtambui Allaah ipasavyo, kwa sababu hawakumthibitishia majina na sifa Zake yanayolingana Naye na ambayo yametajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah. Wanajenga utambuzi wao juu ya Allaah kutoka katika falsafa na akili zao hazijui uhalisia wa utambuzi juu ya Allaah (´Azza wa Jall).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 93-94
  • Imechapishwa: 12/08/2024