56. Ibn ´Abdil-Wahhaab kuhusu kumkufurisha anayemwomba asiye Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ‘Abdul-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ikiwa sisi hatuwakufurishi wale walioliabudu sanamu lilioko juu ya kaburi la ‘Abdul-Qaadir, na sanamu lilioko juu ya kaburi la Ahmad al-Badawiy na mfano wao kwa sababu ya ujinga wao na kutokuwapo wa kuwatahadharisha, basi vipi tutamkufurisha yule ambaye hakumshirikisha Allaah kwa kuwa hakuhamia kwetu au hakuwakufurisha na kuwapiga vita? Kutakasika ni Kwako, hili ni uzushi mkubwa!”[1]

Amesema pia:

“Bali tunamshuhudisha Allaah juu ya anachokijua katika nyoyo zetu kuwa mwenye kutekeleza Tawhiyd na kujitenga mbali na shirki na watu wake, huyo ni muislamu katika zama zozote na mahali popote. Hakika hapana vyengine sisi tunamkufurisha yule aliyemshirikisha Allaah katika ´ibaadah Yake baada ya kumbainishia hoja juu ya upotovu wa ushirikina.”[2]

Amesema pia:

“Kile kilichotajwa kwenu kuwa mimi ninakufurisha kwa jumla, basi hiki ni uzushi wa maadui. Vilevile maneno yao kuwa nasema: ”Mwenye kufuata dini ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akakaa katika mji wake haitoshi mpaka aje kwangu”, basi hii pia ni uzushi. Kilichokusudiwa ni kufuata dini ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika ardhi yoyote. Lakini tunamkufurisha yule anayekiri dini ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha akaipinga na akawazuia watu nayo. Vivyo hivyo anayeyaabudu masanamu baada ya kujua kuwa hiyo ni dini ya washirikina kisha akaipamba kwa watu, huyu ndiye ninayemkufurisha. Kila mwanachuoni duniani humkufurisha mtu wa namna hii, isipokuwa mtu mpinzani au mjinga.”[3]

Amesema pia:

“Ama yale waliyoyataja maadui kunihusu kuwa ninakufurisha kwa dhana na kwa uungaji mkono au ninamkufurisha mjinga ambaye bado hajafikishiwa hoja, basi hili ni uzushi mkubwa ambao wanakusudia kuwafanya watu wakimbie dini ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[4]

Shaykh ‘Abdul-Latwiyf bin ‘Abdir-Rahmaan bin Hasan Aali ash-Shaykh amesema katika kitabu ”Minhaaj at-Ta’siys wat-Taqdiys”, uk. 98-99:

“Shaykh Muhammad (Rahimahu Allaah) alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na tahadhari kubwa na kukufurisha hovyo, kiasi kwamba hakuamua moja kwa moja kumkufurisha mjinga anayemuomba asiye Allaah miongoni mwa waabudia makaburi au wengineo ikiwa hakupata mtu wa kumnasihi na kumfikishia hoja ambayo mtu hukufurishwa kwa kuiacha. Amesema katika baadhi ya barua zake: ”Na ikiwa sisi hatupigani vita na wanaoabudu kuba ya al-Kuwaaz mpaka tuwafikishie ulingano wa kumtakasia Allaah ´ibaadah, basi vipi tumkufurishe yule ambaye hakuhamia kwetu ilhali yeye ni muumini na mpwekeshaji?”

Amesema: “Aliulizwa kuhusu watu wa namna hiyo miongoni mwa wajinga, akaeleza kwamba yule ambaye amefikishiwa hoja na ana uwezo wa kuielewa, basi anakufurishwa kwa kuabudu makaburi.”

Amesema pia (Rahimahu Allaah) katika ”Miswbaah-udh-Dhwulaam”, uk. 499:

“Basi yule ambaye amefikiwa na ulingano wa Mitume kuhusu kumpwekesha Allaah na ulazima wa kujisalimisha Kwake, kisha akaelewa kuwa Mitume walikuja kwa lengo hili, hana udhuru wa kupingana nao na kuacha kumuabudu Allaah. Huyu ndiye anayehukumiwa kuwa kafiri ikiwa atamuabudu asiyekuwa Allaah na akaweka washirika na miungu pamoja Naye. Shaykh pamoja na wengine miongoni mwa waislamu hawasiti katika hili. Shaykh wetu (Rahimahu Allaah) ameliweka jambo hili wazi na amelieleza kwa kufuata wanavyuoni wa ummah na kwa kuwafuata. Hakumkufurisha yeyote isipokuwa baada ya kusimamisha hoja na kudhihiri kwa dalili. Hadi kwamba yeye (Rahimahu Allaah) alisita katika kumkufurisha mjinga miongoni mwa waabudu wa makaburi ikiwa hakuweza kupatikana mtu wa kumkumbusha. Na hili ndilo lililokusudiwa na maneno yake Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaahu) pale aliposema:

”… mpaka ibainike kwao yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Basi pindi kuwepo kwa maelezo ambayo mzungumziwa anayaelewa na kuyafahamu, hapo imebainika kwake.”

Amesema pia katika ”Miswbaah-udh-Dhwulaam”, uk. 516:

“Shaykh wetu (Rahimahu Allaah) hakumkufurisha yeyote kwa kuanza kwa sababu tu ya kitendo chake au shirki yake, bali alisita katika hilo mpaka athibitike kuwepo kwa hoja ambayo mtu hupewa hukumu ya kufuru kwa kuiacha, jambo ambalo liko wazi katika maneno yake sehemu kadhaa na barua zake kuhusu hilo zinajulikana.”

[1] ad-Durar as-Saniyyah (1/66).

[2] Majmuuu’ Mu’allafaati Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab (3/34).

[3] Majmuu’ Mu’allafaat-ish-Shaykh  (3/33).

[4] Majmuu’ Mu’allafaat-ish-Shaykh (3/14).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 74-78
  • Imechapishwa: 01/07/2026