56. Hakuna yeyote ana haki ya kujiamulia yaliyo mazuri na yaliyo mabaya

Muislamu apate mazingatio juu ya yale yaliyosemwa na Allaah (Ta´ala) kuhusu manaswara:

ثُمَّ قَفَّيْنَا عَلَىٰ آثَارِهِم بِرُسُلِنَا وَقَفَّيْنَا بِعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ وَآتَيْنَاهُ الْإِنجِيلَ وَجَعَلْنَا فِي قُلُوبِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ رَأْفَةً وَرَحْمَةً وَرَهْبَانِيَّةً ابْتَدَعُوهَا مَا كَتَبْنَاهَا عَلَيْهِمْ إِلَّا ابْتِغَاءَ رِضْوَانِ اللَّـهِ فَمَا رَعَوْهَا حَقَّ رِعَايَتِهَا ۖ فَآتَيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا مِنْهُمْ أَجْرَهُمْ ۖ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ

”Kisha Tukafuatisha baada yao Mtume Wetu na tukamfuatisha ‘Iysaa mwana wa Maryam na tukampa Injiyl na tukajaalia ndani ya nyoyo za wale waliomfuata upole na huruma na utawa wameuzusha wao wenyewe hatukuwaandikia hayo juu yao isipokuwa kutafuta radhi za Allaah. Lakini hawakuuchunga ipasavyo kuchungwa. Basi tukawapa wale walioamini miongoni mwao ujira wao – na wengi wao ni mafasiki.”[1]

Wao wenyewe wamejizulia utawa kwa lengo la ´ibaadah. Allaah hakuwaandikia wala hakuwafaradhishia nayo. Bali wao wenyewe ndio walilazimiana nayo kwa ajili ya kutaka kumridhisha Allaah (Subhaanah). Tazama ni namna gani Allaah alivyowachukia na akawasema vibaya licha ya nia yao njema ya kumwabudu Allaah kwa ´ibaadah iliyozuliwa. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) hawataki waja Wake wamwabudu kwa njia nyingine isipokuwa ile ambayo aliiweka katika Shari´ah Yake kupitia Mitume Wake. Hivyo ndio huonekana ukweli wa wale wenye kumuitikia Allaah na Mtume Wake pale anapowaita katika yale yanayowapa uhai. Kama ambavyo Allaah hayakubali matendo ya mshirikina, bila kujali namna yalivyo mengi, vivyo hivyo hayakubali matendo ya mzushi, bila kujali namna yalivyo mengi. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِن لَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكَ فَاعْلَمْ أَنَّمَا يَتَّبِعُونَ أَهْوَاءَهُمْ ۚ وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّنِ اتَّبَعَ هَوَاهُ بِغَيْرِ هُدًى مِّنَ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ

“Na wasipokuitikia, basi tambua kwamba hakika wanafuata matamanio yao. Na nani mpotofu zaidi kuliko yule aliyefuata matamanio yake pasi na uongofu kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah hawaongozi watu madhalimu.”[2]

Si kila mtu ana haki ya kufuata yale anayoyapenda, akayaamrisha na kuyafanya kuwa ni dini, au akakataza yale anayoyachukia na akayasimanga na kuyafanya kuwa ni dini, isipokuwa kwa mwongozo kutoka kwa Allaah – na mwongozo wa Allaah ni ile Shari´ah Yake ambayo amemtumiliza Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwayo. Yeyote mwenye kupenda na kuchukia kwa matamanio yake na si kwa mujibu wa Shari´ah, basi ameyafuata matamanio yake pasi na mwongozo wa Allaah. Ni ufuataji wa matamanio upi ulio mbaya zaidi kushinda kupuuzilia mbali ule mfumo wa ulinganizi uliowekwa na Allaah (Ta´ala) na kwenda katika mifumo ya ulinganizi iliyozuliwa! Hivyo ni kwa sababu yule mtendaji anadhani kuwa inamkurubisha kwa Allaah na ni ´ibaadah, ilihali ukweli wa mambo ni kuwa ndio upotofu wenyewe na msingi wa maharibifu. Allaah (Ta´ala) amesema kweli pale aliposema:

وَمَن يَعْشُ عَن ذِكْرِ الرَّحْمَـٰنِ نُقَيِّضْ لَهُ شَيْطَانًا فَهُوَ لَهُ قَرِينٌ وَإِنَّهُمْ لَيَصُدُّونَهُمْ عَنِ السَّبِيلِ وَيَحْسَبُونَ أَنَّهُم مُّهْتَدُونَ

”Anayejifanya kipofu na ukumbusho wa Mwingi wa rehema, basi Tunamwekea shaytwaan awe ndiye rafiki yake mwandani. Na hakika wao [mashaytwaan hao] wanawazuia njia na wanadhania kwamba wao wameongoka.”[3]

[1] 57:27

[2] 28:50

[3] 43:36-37

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 81-82
  • Imechapishwa: 28/05/2023