Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

47 – Kwa haki kabisa waumini wamesadikisha jambo hilo na kuyakinisha kuwa ni maneno ya Allaah kikweli.

MAELEZO

Wale wanaomwamini Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanasadikisha kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mfikishaji tu kutoka kwa Allaah.

Kuhusu maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ

“Hakika hii bila shaka ni kauli ya Mjumbe mtukufu. Mwenye nguvu na cheo kitukufu kwa Mwenye kumiliki ‘Arshi.”[1]

maana yake ni kwamba Jibriyl ndiye ameyafikisha. Kwa sababu haiwezekani Qur-aan ikawa ni maneno ya Allaah na wakati huohuo ikawa ni maneno ya Jibriyl. Maneno hayawezi kutoka isipokuwa kwa mtu mmoja na hayawezi kunasibishwa kwa zaidi ya mtu mmoja. Wakati Qur-aan inanasibishwa kwa Allaah, ni kwa njia ya uhakika, ama kunasibishwa kwa Jibriyl, ni kwa njia ya kuifikisha.

Imekuja katika Aayah nyingine:

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ وَمَا هُوَ بِقَوْلِ شَاعِرٍ ۚ قَلِيلًا مَّا تُؤْمِنُونَ

“Hakika hii bila shaka ni kauli ya Mtume mtukufu, na si kauli ya mshairi; ni machache mno yale mnayoamini.”[2]

Aayah inamlenga Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maneno yameegemezwa kwake kwa njia ya ufikishaji. Wakati fulani Allaah ameiegemeza Qur-aan Kwake Mwenyewe, wakati mwingine ameiegemeza kwa Jibriyl na wakati mwingine ameiegemeza kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo maneno hayawezi kuzungumzwa na zaidi ya mtu mmoja. Kwa hiyo pindi maneno yananasibishwa kwa Allaah, ni kwa njia ya uhakika, na pindi yanaegemezwa kwa Jibriyl na Kuhammad, ni kwa njia ya ambaye ameyafikisha.

[1] 81:19-20

[2] 69:40-41

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 68
  • Imechapishwa: 11/01/2023