Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

46 – Kwake ndio imeanza kwa njia ya maneno, jambo ambalo halitakiwi kufanyiwa namna, na Akaiteremsha kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia ya Wahy.

MAELEZO

Qur-aan imeteremshwa kutoka kwa Allaah. Allaah ameongea kwayo na akaiteremsha. Haikushuka kutoka kwa mwingine na wala haikuanza kutoka kwa mwingine. Haikuanza kutoka kwa Jibriyl, Ubao wala hewani. Mwanzo wake ni kutoka kwa Allaah, Jibriyl akaisikia na akamfikishia nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia ya Wahy. Laiti kama Qur-aan ingelikuwa inatoka kwa mtu basi angeliweza yeyote kuandika Suurah moja mfano wake. Wakati waliposhindwa kufanya hivo ikafahamisha kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Ta´ala):

وَإِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Mkiwa mko katika shaka kutokana na Tuliyoyateremsha juu ya mja Wetu, basi leteni Suurah mfano wake na waiteni mashahidi wenu pasipo na Allaah mkiwa ni wakweli.”[1]

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ فَأْتُوا بِعَشْرِ سُوَرٍ مِّثْلِهِ مُفْتَرَيَاتٍ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

”Je, wanasema ameitunga [hii Qur-aan]? Sema: ”Leteni Suurah kumi mfano wake zilizotungwa na iteni muwawezao pasi na Allaah mkiwa nyinyi ni wakweli.”[2]

Allaah akathibitisha kushindwa kwao, licha ya kuwa wao ni waarabu tena wafasaha na Qur-aan imeandikwa kwa kiarabu na kwa herufi ambazo wao wanazungumza. Walikuwa ni wenye kupupia kumfanyia inda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wangeliweza kuipa changamoto Qur-aan hii basi wasingesita hata kidogo kufanya hivo. Lakini waliposhindwa kufanya hivo, basi ikajulisha kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah.

[1] 2:23

[2] 11:13

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 67-68
  • Imechapishwa: 11/01/2023