Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili kutoka katika Sunnah ni Hadiyth ya Jibriyl inayojulikana iliyopokelewa na ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Siku moja tulipokuwa tumekaa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutokea mtu ambaye nguo zake zilikuwa nyeupe pepe na nywele zake zilikuwa nyeusi sana. Hakuwa na alama ya kuonesha kuwa ni msafiri na wala hapakuwa na hata mmoja katika sisi aliyemtambua. Alienda akakaa karibu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaweka magoti yake karibu na magoti yake na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake.” Akasema: “Ee Muhammad, nieleze kuhusu Uislamu!” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Uislamu ni kushuhudia kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji Nyumba kwa yule mwenye uwezo wa kuiendea.”

MAELEZO

Hadiyth hii ndefu – inatambulika kama Hadiyth ya Jibriyl – ameisimulia ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) kwa kirefu na ameipokea Imaam Muslim katika ”as-Swahiyh” yake. Katika Hadiyth hii kumebainishwa ngazi tatu za Uislamu; ngazi ya Uislamu, ngazi ya imani na ngazi ya Ihsaan. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) tayari amekwishatangulia kutaja dalili zake kutoka ndani ya Qur-aan na hivi sasa ametaja dalili zake kutoka katika Sunnah.

Hadiyth hii ni tukufu. Wanazuoni wameipokea kwa kuikubali na wakaifafanua. Endapo itapambanuliwa kwa kina basi maelezo yake yangelikuwa katika mijeledi mingi mikubwamikubwa kutokana na ile elimu iliyomo ndani yake.

Maneno yake (Radhiya Allaahu ´anh):

“… na wala hapakuwa na hata mmoja katika sisi aliyemtambua.”

Bi maana tukashangazwa ni vipi anakuja mtu wa ajabu ambaye hakuna yeyote katika sisi anayemtambua. Licha ya hili ni nguo zake ni nyeupe pepe, nywele zake ni nyeusi sana. Kipindi hicho kutokana na ugumu wa usafiri wa ngamia na kadhalika msafiri alikuwa akifika na nguo zilizochakaa, nywele timtim na nguo zimechafuka. Mambo haikuwa kama safari zetu za leo kwa ndege, meli na treni. Bwana huyu alikuwa alikuwa msafiri na mgeni. Hakuwa miongoni mwa watu wa mji na wala hakuwa na alama ya safari. Bwana huyu alikuwa Jibriyl (´alayhis-Salaam). Alikuwa katika sura ya mtu. Hata hivyo wakati alipokuja Maswahabah hawakuwa wakimtambua.

Maneno yake (Radhiya Allaahu ´anh):

”Alienda akakaa karibu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaweka magoti yake karibu na mago yake… “

Alikaa mbele ya Mtume kikao cha heshima. Akaweka magoti yake karibu na magoti ya Mtume na viganja vyake juu ya mapaja yake hali ya kumuuliza.  Imepokelewa katika baadhi ya matamshi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye alisema:

“Niulizeni ambapo wakamuogopa.”[1]

Ndipo Allaah akamtuma Jibriyl alimuulize ili Maswahabah wafaidike.

[1] Muslim (10).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 72-73
  • Imechapishwa: 14/02/2023