53. Nguzo ya kumi na moja ya swalah ni kusoma Tashahhud ya mwisho

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tashahhud ya mwisho ni nguzo na ni wajibu kama ilivyo katika Hadiyth ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kabla hatujafaradhishiwa Tashahhud tulikuwa tukisema: “Salaam zimwendee Allaah kutoka kwa waja Wake, salaam zimwendee Jibriyl na Miykaaiyl.” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Hapana kusema “Salaam zimwendee Allaah kutoka kwa waja Wake, kwani hakika Allaah ni ndiye as-Salaam (Mwenye kutoa amani). Lakini semeni:

التحيات لله، و الصلوات و الطيبات، السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته، السلام علينا و على عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله و أشهد أن محمداً عبده و رسوله

“Maadhimisho, swalah na mazuri yote yanamstahikia Allaah. Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume! Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”

التحيات لله

maadhimisho yote yanamstahiki Allaah kwa njia inayolingana na Ukubwa na Utukufu Wake, kama Rukuu´, Sujuud na kudumu milele. Vyote ambavyo Mola wa walimwengu huadhimishwa kwavyo, vinamstahiki Allaah. Atakayemfanyia katika hayo chochote asiyekuwa Allaah ni mshirikina kafiri.

الصلوات

Maana yake ni du´aa zote na imesemekana kuwa maana yake ni zile swalah tano.

الطيبات

Allaah ni Mzuri na wala hayakubali maneno na vitendo isipokuwa mazuri tu.

السلام عليك أيها النبي ورحمة الله وبركاته

”Amani iwe juu yako, ee Mtume, rehema na baraka za Allaah.”

Wamuombea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amani, rehema na baraka. Anaombewa, na wala haombwi pamoja na Allaah.

السلام علينا و على عباد الله الصالحين

“Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah.”

Wajiombea amani mwenyewe na kwa kila kiumbe mwema katika mbingu na ardhi. as-Salaam ni du ´aa huombewa waja wema lakini haitakiwi kuwaomba wao pamoja na Allaah.

أشهد أن لا إله إلا الله و أشهد أن محمداً عبده و رسوله

“Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”

Unashuhudia shahaadah ya yakini ya kwamba hakuna anayestahiki kuabudiwa kwa haki katika ardhi wala mbinguni isipokuwa Allaah. Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ina maana ni mja asiyeabudiwa na ni Mtume asiyekadhibishwa, bali anatiiwa na kufuatwa. Allaah kamtukuza kwa kuwa mja. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَى عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا

“Amebarikika Yule ambaye ameteremsha Pambanuzi kwa mja Wake ili awe ni muonyaji kwa walimwengu.”[1]

MAELEZO

Tashahhud inayokuwa kabla ya salamu katika kila swalah ni nguzo miongoni mwa nguzo za swalah. Hii ndio nguzo ya kumi na moja. Nguzo ya kumi na mbili ni kukaa katika Tashahhud hiyo. Ikiwa mtu atatoa salamu baada ya kusujudu, basi atakuwa ameacha nguzo mbili. Ikiwa ataketi na akasahau kuleta Tashahhud, basi ameacha nguzo moja. Kuacha viwili vyote au kuacha Tashahhud pekee, kunabatilisha swalah. Tashahhud imepokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa matamshi mbalimbali. Inatosha kutekeleza wajibu kwa yoyote katika matamshi hayo. Mtu asikufanye matamshi yote hayo katika swalah moja.

Tashahhud iliotajwa na Shaykh ni Tashahhud ya ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh). Katika baadhi ya mapokezi yake imekuja ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anawafundisha kama anavyowafundisha Suurah ndani ya Qur-aan. Imeitwa ”Tashahhud” kwa sababu inamalizia kwa:

“Nashuhudia ya kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kuwa Muhammad ni mja wake na Mtume wake.”

Tashahhud hii ameipokea al-Bukhaariy (831) na Muslim (402). Kumepokelewa ziada kwa al-Bukhaariy (6265) baada ya kutaja Tashahhud:

“… wakati alikuwa kati yetu. Alipoaga dunia tukawa tunasema: ”Amani… ” kwa maana juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Maana ni kwamba Maswahabah walikuwa wakisema:

السلام عليك أيها النبي ورحمة الله وبركاته

”Amani iwe juu yako, ee Mtume, rehema na baraka za Allaah.”

Kwa namna ya kumzungumzisha. Lakini alipofariki walikuwa wakisema:

السلام على النبي

”Amani iwe juu ya Mtume… ”

Kwa kutumia tamko la kutajwa mtu aliyepo mbali. Hata hivyo imekuja katika Tashahhud ya ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) katika ”al-Muwattaa´” (53) ya Imaam Maalik kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Abdil-Qaariy ya kwamba alimsikia ´Umar bin al-Khattwaab akiwa juu ya mimbari akiwafundisha watu Tashahhud hali ya kusema: “Semani:

التحيات لله

”Mamkuzi kwa Allaah… ”

ambapo ndani yake imekuja:

السلام عليك أيها النبي ورحمة الله وبركاته

”Amani iwe juu yako, ee Mtume, rehema na baraka za Allaah.”

Kwa mtindo wa kuzungumzishwa. Kwa hiyo katika hili kuna ya kwamba ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akifundisha Tashahhud akiwa juu ya mimbari. Miongoni mwa alichokifundisha ni tamko hili.

Jengine ni kwamba inajulisha ya kwamba Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum), baada ya kufariki kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kumepokelewa kutoka kwao yote mawili. Kwa msemo mwingine kuna wasaa katika jambo hilo. Kwa hiyo mswaliji aseme:

السلام عليك أيها النبي ورحمة الله وبركاته

”Amani iwe juu yako, ee Mtume, rehema na baraka za Allaah.”

Pia anaweza kusema:

السلام على النبي ورحمة الله وبركاته

”Amani iwe kwa Mtume, rehema na baraka za Allaah.”

Shaykh (Rahimahu Allaah) amefafanua Tashahhud hii kwa maelezi haya ya wazi. Maneno yake Shaykh (Rahimahullaah):

السلام عليك أيها النبي ورحمة الله وبركاته

”Amani iwe juu yako, ee Mtume, rehema na baraka za Allaah.”

kwa manaa ya kwamba unamwombea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) salama, rehema na baraka. Yule anayeombewa du´aa haombwi pamoja na Allaah.

[1] 25:01

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 63-68
  • Imechapishwa: 01/07/2026