Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Halafu mtu anaenda kwenye Rukuu´, kuinuka kutoka kwenye Rukuu´, kunyooka sawasawa, kusujudu juu ya viungo saba na kuinuka kutoka hapo na kukaa baina ya Sujuud mbili. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا

 “Enyi mloamini! Rukuuni na sujuduni.”[1]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimeamrishwa kujusudu juu ya viungo saba.”[2]

Ni lazima kuwa na utulivu katika vitendo vyote na kupangilia kati ya kila nguzo. Dalili ni Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah kuhusiana na mtu aliyekuwa akiswali vibaya. Kasema:

“Wakati tulipokuwa tumekaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuliingia mtu, akaswali kisha akamsalimia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akamwambia “Rudi ukaswali, hakika hujaswali.” Alifanya hivi mara tatu. Mwishoni akamwambia: “Naapa kwa yule aliyekutuma kwa haki; siwezi bora zaidi ya hivi. Nifunze!” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Unaposimama kutaka kuswali, lete Takbiyr. Kisha soma uwezacho katika Qur-aan. Kisha utarukuu mpaka unyooke. Kisha utasimama sawa sawa. Kisha utasujudu mpaka utapotulia katika sujuud. Kisha utainuka na kutulia katika kikao kisha utafanya hivyo katika swalah zote.”

MAELEZO

Hizi ni saba miongoni mwa nguzo za swalah ambazo zote ni vitendo. Zote hizo zimejulishwa na Hadiyth ya yule bwana aliyefanya vibaya katika swalah yake. ameipokea al-Bukhaariy (757) na Muslim (397) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

Hadiyth ya kusujudu juu ya viungo saba ameipokea al-Bukhaariy (812) kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimeamrishwa nisujudu juu ya viungo saba: juu ya kipaji cha uso – na akaashiria kwa mkono wake kwenye pua yake – na juu ya mikono, magoti na ncha za nyayo mbili na wala tusifunge nguo na nywele.”

Ameipokea pia Muslim (490).

Kufanya utulivu katika nguzo. Ni kuwa mtulivu na kutofanya haraka. Kwa maana ya kwamba mtu asifanye pupa na haraka katika vitendo hivi, bali awe mtulivu ndani yake, ni mamoja iwe ni kwa muda mrefu au mfupi.

Kuhusu kufanya kwa mpangilio anapaswa kuvifanya kwa mpangilio; kusimama, kisha kurukuu, kisha kuinuka kutoka hapo, kisha kusujudu, kisha kuketi kati ya sujuud mbili. Kwa mfano akisujudu kwa kusahau kabla ya kurukuu, ni lazima arejee ili afanye Rukuu´ kisha Sujuud. Asizingatie ile Sujuud aliyoifanya kwa sababu ya kusahau.

[1] 22:77

[2] al-Bukhaariy (810) na Muslim (490).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 61-63
  • Imechapishwa: 01/07/2026