53. Je, ni wajibu kutahadharisha kutokana na mifumo inayoenda kinyume na mfumo wa Salaf?

Swali 53: Je, ni wajibu kutahadharisha kutokana na mifumo inayoenda kinyume na mfumo wa Salaf?

Jibu: Ndio. Ni lazima tutahadharishe mifumo inayopingana na mfumo wa Salaf[1]. Kufanya hivo ni katika kumtakia mema Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, viongozi wa waislamu na watu wao wa kawaida.

Tunatahadharisha kutokana watu waovu. Tunatahadharisha na mifumo inayopingana na mfumo wa Kiislamu. Tuyabainishe madhara ya mambo haya kwa watu. Tuwahimize kushikamana na Qur-aan na Sunnah. Hili ndio la wajibu.

Lakini hii ni kazi inayofanywa na wanazuoni ambao ndio wanaotakiwa kuyaingilia mambo haya na wawawekee nayo watu wazi kwa njia ya sawa, iliyowekwa katika Shari´ah na iliyofanikiwa kwa idhini ya Allaah.

[1] Huu ndio mfumo wa Salaf. Walikuwa (Rahimahumu Allaah) ni wakali katika kutahadharisha mifumo inayopingana na Qur-aan na Sunnah. Bali walikuwa wakiwaingilia hata wale wanaowatukuza wao au vitabu vyao. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Ni wajibu kumuadhibu yule anayejinasibisha kwao, akawatetea, akawasifia, akavitukuza vitabu vyao, anatambulika kuwasaidia au kuwanusuru, kuchukia pindi wanapozungumzwa au akawapa udhuru na kusema kuwa maana ya maneno yao haijulikani, akahoji usahihi wa kitabu hicho na mfano wa nyudhuru kama hizo ambazo hazisemwi isipokuwa na mjinga au mnafiki tu. Bali ni wajibu kwa kila ambaye anazitambua hali zao kuwaadhibu. Ni miongoni mwa wajibu mkubwa kabisa kusimama kidete dhidi ya watu hawa.” (Majmuu´-ul-Fataawaa (2/132))

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 144-145
  • Imechapishwa: 06/03/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy