52. Walinganizi wanaoharibu zaidi kuliko wanavyotengeneza na mwamko wa Kiislamu

Swali 52: Kunaonekana kutoka kwa baadhi ya vijana wa Muamko[1] wanakuwa na shauku kubwa ya kulingania kutokana na yale wanayosikia juu ya malipo makubwa ya mlinganizi. Kisha haraka sana hamasa hiyo inaondoka. Ni zipi nasaha zako juu ya hilo?

Jibu: Mimi ninanyamaza inapokuja katika istilahi ya ´muamko wa kiislamu` (الصحوة الإسلامية). Limeenea katika magazeti zaidi ya mara moja. Istilahi hiyo inakanusha ile juhudi kubwa iliyowekwa na wanazuoni wanaotengeneza katika nyakati zote na aina nyenginezo zote za juhudi zilizopo katika ummah huu. Ni jambo litaloendelea kuwepo ardhini mpaka kisimame Qiyaamah.

Ni vizuri kuwa na shauku juu ya kulingania. Mtu anaweza kuwa na hamu ya kufanya kheri na kulingania. Lakini haijuzu kwake kuanza kulingania isipokuwa baada ya kujifunza. Atambue ni vipi atalinganie kwa Allaah (´Azza wa Jall) na azijue njia za kulingania. Awe na utambuzi wa kile anacholingania kwacho:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata.”[2]

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi… ”[3]

Bi maana kutokana na utambuzi.

Mjinga hafai kulingania. Ni lazima kwanza awe na elimu, kumtakasia Allaah nia, subira, kustahamili na hekima. Aidha ni lazima pia ajue namna atalingania na mifumo ya ulinganizi aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ama kuwa na hamasa peke yake au kupenda ulinganizi na akaanza kulingania, ukweli wa mambo ni kwamba huharibu zaidi kuliko anavyotengeneza. Anaweza kuingia katika matatizo na kuwaingiza wengine ndani ya matatizo. Mtu kama huyu inatosha kwake akawapendezeshea watu kheri. Analipwa thawabu kwa hilo – Allaah akitaka. Lakini kama anataka kuingia katika uwanja wa ulinganizi basi aanze kusoma kwanza. Si kila mwenye shauku anasilihi kulingania. Hamasa zinazotokana na ujinga zinadhuru na wala hazinufaishi[4].

[1] Istilahi ´muamko` au ´vijana wa muamko` na ´muamko wa kiislamu` linakaririwa mara nyingi na baadhi ya walinganizi na vijana. Linatoa hisia kwamba ummah wa kiislamu walikuwa wamelala au walikuwa kwenye koma na hawakuwa na ulinganizi. Si kweli. Kwa sababu waislamu na khaswa katika nchi hii kheri daima ilikuwepo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hatokuacha kuwepo kikundi kutoka katika ummah wangu hali ya kuwa ni chenye kushinda juu ya haki.”

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Ummah wangu haukusanyiki juu ya upotevu.” (Kashf-ul-Khifaa’ (2999) na Tadhkirat-ul-Muhtaaj (51))

Ummah wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado siku zote uko macho na umesimama. Wanazuoni wapo katika kila zama, kizazi baada ya kizazi. Haijapatapo kuwepo kipindi fulani bila mwanachuoni. Tukisema kinyume na hivo basi tutakuwa tumekadhibisha maneno yake mteule (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hatokuacha kuwepo kikundi kutoka katika ummah wangu hali ya kuwa ni chenye kushinda juu ya haki. Hakitodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura wala wale wenye kwenda kinyume nao mpaka ifike amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) wakiwa katika hali hiyo.” (Muslim (3/1037))

Wale wanaozungumzia muamko na historia yake wanatoka katika kipote cha leo al-Ikhwaan al-Muslimuun kilichoungwa Misri na al-Hasan al-Bannaa. Hayo yanatiliwa nguvu na Muhammad Qutwb na wengineo. Amesema katika ”Waaqiy´unaa al-Muaaswir”:

”Sisi tunasoma jambo hilo ´muamko wa kiislamu`. Lilianza kwenye moyo wa mtu mmoja (bi maana Hasan al-Bannaa). Allaah alimfungulia na akamtunuku mng´aro wa roho na mawasiliano masafi na Allaah.”

Namna hii husema Suufiyyah. Himdi zote njema ni stahiki ya hakusema kuwa alisoma chini ya wanazuoni wanaotambulika. Lingewadanganya watu wa kawaida na kumuona kuwa ni mwanachuoni. Watu wenye busara hawawaamini isipokuwa tu wanazuoni tofauti na wajinga ambao wanamuamini kila mtu. Amesema tena:

”Mng´aro huu ndani ya moyo na roho ya Hasan al-Bannaa ilikuwa ni ushindi wa kiungu… Wakati huohuo ilikuwa ni muitiko sahihi wa matokeo yote yaliyotokea kwa zaidi ya karne moja iliyopita katika ulimwengu wote wa Kiislamu na khaswa Misri.” (Uk. 403)

Maneno haya yanafahamisha kuwa mwanzoni mwa ulinganizi wa al-Ikhwaan al-Muslimuun ilikuwa ni pingamizi tupu. Wanalijua wao wenyewe. Muhamamd Qutwub ameandika kitabu kwa jina ”as-Swahwah al-Islaamiyyah”. Mchapishaji amesema katika utangulizi wake:

”Uamsho wa Kiislamu ambao umeangazia ulimwengu wa Kiislamu unazingatiwa kuwa jambo kubwa zaidi ambalo limetokea kwa mwanadamu katika nusu ya pili ya karne ya 20.”

Muhammad Qutwub amesema:

“Ingawa mwamko wa Kiislamu umewashangaza watu hapa na pale, umekuja kwa mujibu wa wakati uliowekwa na Allaah.” (Uk. 75)

Hapana shaka ya kwamba kila kitu kimekadariwa na Allaah. Hata hivyo hakuna kheri yoyote katika mwamko huu. Kuna mshangao gani ndani yake?

Amesema tena:

“Harakati ya imamu na shahidi ilikuja wakati karibu ummah wote ulikuwa umelala.” (Uk. 63)

Amesema tena:

”Makundi yanayofanya kazi yanatofautiana hii leo… juu ya mfumo wa kiharakati ambao ni lazima kuufuata… Harakati zilikuwa zikiafikiana na mfumo uliowekwa na imamu na shahidi na ambao ameliunda kundi lake juu yake. Hakukuwepo kundi lingine zaidi ya kundi hilo.” (Uk. 96)

Uko wapi ulinganizi wa Salafiyyah Saudi Arabia na kwenginepo? Ambao kipindi hicho – na hata hii leo – ndio ulikuwa na nguvu zaidi. Mpaka hii leo waislamu wote wanavuna matunda yake yaliyobarikiwa. Tofauti na linganizi zingine zote hakuna ndani yake kitu hasi. Watu hawa wanaingia ndani ya maneno ya mshairi:

Haki ni jua na macho ni maono

lakini hujificha kwa vipofu

Au maneno ya mtu mwengine aliyesema:

Jicho linaweza kukataa mwanga wa jua kutokana na maradhi

Mdomo pia unaweza kutohisi ladha ya maji kutokana na maradhi

Bakr Abu Zayd amesema katika kitabu chake ”Mu´jam-ul-Manaahiy al-Lafdhwiyyah” wakati alipokuwa anaongelea mada ya ´mwamko wa Kiislamu`:

”Haya ni maelezo ambayo Allaah hakuyafungamanishia hukumu yoyote. Kwa hivyo ni istilahi iliyozuka. Wala hatutambui kuwa ilitumiwa na Salaf. Ilitumiwa mwanzoni mwa karne ya kumi na tano baada ya kuhajiri wakati ambapo manaswara na wengineo walirudi kanisani. Kisha baada ya hapo ndio ikaenda kwa waislamu. Haifai kwa waislamu kuwaigiliza katika mambo ya kidini. Hawatakiwi kuchukua nembo ambazo hazikuidhinishwa na Allaah wala Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Majina yaliyowekwa katika Shari´ah yanajengeka juu ya Qur-aan na Sunnah peke yake: Uislamu, imani, ihsaan na taqwa na muslim, mu´min, muhsin na taqiy´.  Laiti ningejua ni wapi umetoka uzushi huu wa ´mwamko wa Kiislamu`. Umetokana na ´mwamko` (صاحٍ) au nini?

[2] 12:108

[3] 12:108

[4] Dhiraar bin ´Amr amesema:

”Naapa kwa ambaye hakuna mungu wa haki mwingine isipokuwa Yeye ya kwamba hakuna mtu ambaye aliteda kwa ujinga isipokuwa ilikuwa yale aliyoyaharibu ndio mengi kuliko aliyotengeneza.” (al-Faqiyh wal-Mutaffaqih (1/19))

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 140-144
  • Imechapishwa: 05/03/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy