Swali 51: Kipi unawachowanasihi wanafunzi wanaoanza?

Jibu: Nawanasihi wanafunz wanaoanza kusoma kwa wanazuoni[1] wanaoaminika kwa ´Aqiydah, elimu na kuwatakia kwao watu mema. Nawanasihi waanze na vitabu vilivyoandikwa kwa ufupi, wavihifadhi na wasome maelezo kutoka kwa waalimu wao hatua kwa hatua. Hili khaswa vitabu vya mtaala kutoka katika mataasisi na vyuo vikuu. Kuna kozi nyingi za kielimu ambazo mwanafunzi anazisoma hatua kwa hatua na ni nzuri mno.

Ikiwa mwanafunzi hawezi kupata shule hizi za kiserikali basi atafute elimu kutoka kwa wanazuoni misikitini katika asome Fiqh, sarufi, ´Aqiydah na mengineyo.

Kuhusu yale yanayofanywa na vijana hii leo ambapo wanaanza kusoma vitabu vikubwavikubwa au wananunua vitabu na kukaa nyumbani kwake na kuvisoma, ni jambo lisilofaa. Huku sio kusoma; huko ni kujighuri. Hilo ndilo limepelekea kwa baadhi ya watu kuzungumza juu ya Allaah pasi na elimu, kwa sababu hakujenga juu ya msingi. Ni lazima kukaa na wanazuoni katika mizunguko ya kielimu na ni lazima kuwa na subira.

[1] Hapa ni muhimu kutambulisha nini maana sahihi ya wanazuoni. Kwa sababu ya watu wengi kutofahamu wamewapenyesha watu wengi wasiostahiki katika safu ya wanazuoni. Matokeo yake kukatokea vurugu ya kielimu ambayo hivi sasa tunahisi uchungu wake. Watu wengi wa kawaida kwa jumla na khaswa wanafunzi wanafikiri kuwa kila ambaye anatunga kitabu, ametoa hati ya mkono, Khutbah au ametoa muhadhara, basi huyo ndiye mwanachuoni. Ni wachache mno leo hii wanaostahiki kuitwa wanazuoni. Kwa sababu mwanachuoni anazo sifa ambazo pengine wasiwe nazo watu wengi ambao wanajinasibisha na elimu hii leo. Mwanachuoni sio yule ambaye ni mfaswaha katika Khutbah na mihadhara yake. Wala mwanachuoni sio yule ambaye ameandika kitabu, amehakiki tungo au hati ya mkono kisha akaitoa. Vijana wengi na watu wa kawaida wanamtambua mwanachuoni kwa alama hizo. Haafidhw Ibn Rajab al-Hanbaliy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Tumepewa mtihani wa baadhi ya watu ambao wanaamini kuwa wale waliokuja nyuma wanaozungumza vizuri ni watambuzi zaidi kuliko vile vizazi vilivyotangulia. Miongoni mwao ambao wanafikiri kuwa anayeandika na kuzungumza sana ni mjuzi zaidi kuliko kila aliyetangulia katika Maswahabah na wale waliokuja nyuma yao.”

Amesema tena:

”Watu wengi waliokuja baadaye wamepewa mtihani huu. Wamefikiri kuwa anayezungumza na kubishana sana katika mambo ya dini ndiye mjuzi zaidi kuliko asiyekuwa hivo.”

Hali ilikuwa namna hiyo katika wakati wa Ibn Rajab (Rahimahu Allaah). Angesema nini endapo angeliwaona wale wanaojifunza wanazuoni katika zama zetu hizi ambao wamejaza vitabu na kanda zao kwa maeneno yao? Watu wakadanganyika nao kutokana na zile kanda nyingi wanazotoa kila wiki na kuandika vitabu vipya kila mwezi. Matokeo yake wakadhania wao ndio wanazuoni. Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) amesema tena:

”Ni lazima kuamini kuwa si kila mtu ambaye anazungumza sana katika mambo ya elimu ina maana kuwa ni mjuzi zaidi kuliko ambaye hafanyi hivo.” (Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 38-40)

Miongoni mwa mambo mengine yanayompambanua mwanachuoni hii leo ni utuuzima wake. Ni sharti pia elimu ichukuliwe kutoka kwa wanazuoni wakubwa na khaswa leo hii. Mtumzima elimu yake inakuwa yenye kubobea zaidi, akili kamilifu zaidi na mwenye kulindwa zaidi kutokana na matamanio na mengineyo.” Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Watu wataendelea kuwa katika kheri muda wa kuwa wanachukua elimu kutoka kwa wakubwa, waaminiwa na wanazuoni wao. Wanapochukua elimu kutoka kwa wadogo na waovu wao basi wanaangamia.”

al-Khatwiyb al-Baghdaadiy (Rahimahu Allaah) amepokea kwamba Ibn Qutaybah (Rahimahu Allaah) aliulizwa maana ya upokezi uliotangulia hapo juu akajibu kwa kusema:

”Watu wataendelea kuwa katika kheri muda wa kuwa wanazuoni wao ni watuwazima na si watoto.”

Baada ya hapo akafafanua tafsiri hii na akasema:

”Kwa sababu mtumzima imemuondokea starehe ya ujana, ukali wake, haraka yake na upumbavu wake na badala yake amepata uzoefu na ukomavu. Hivyo katika elimu yake hakuingii shubuha. Matamanio hayamshindi. Havutikiwi na tamaa. Hawi ni mateka ya shaytwaan kama anavofanya kwa kijana. Kwa umri kunakuja utukufu, hadhi na haiba. Chipukizi anaweza kufikwa na mambo yote haya ambayo mtumzima amesalimika nayo. Anapofanya hivo na akatoa fatwa basi huangamia yeye na akaangamiza wengine.” (Naswiyhatu Ahl-il-Ahadiyth, uk. 7)

Ibn ´Abdil-Barr katika kitabu ”Jaamiy´ Bayaan-il-´Ilm wa Fadhwlih” ameweka mlango kamili unaozungumzia ni nani anayestahiki kikweli kuitwa mwanachuoni au mjuzi na ni wanazuoni wepi wanaotakiwa kutoa fatwa. Arejee huko yule anayetafuta elimu na haki, kwani ni muhimu – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 137-140
  • Imechapishwa: 05/03/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy