Yule ambaye hii leo atashikana barabara na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akazitendea kazi, akawa na msimamo kwazo na akalingania kwazo,  basi malipo yake yanakuwa mengi na makubwa zaidi kuliko ya wale wenzao kati ya wlae waliotangulia katika Uislamu. Kwa sababu Mtume mteule (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mbele yenu kunakuja masiku ambayo mwenye subira ni kama mfano wa aliyeshika kaa [la moto] na mtendaji mwenye kutenda kama nyinyi analipwa ujira wa wanaume khamsini.” Tukasema: “Katika sisi au katika wao?” Akasema: “Katika nyinyi.”[1]

Ameyasema hayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu wale watu ambao wanatendea kazi Sunnah zake wakati ummah wake umeharibika.

Nimepata kwenye kitabu cha babu yangu, Shaykh na Imaam Abu ´Abdillaah Muhammad bin ´Adiy bin Hamduuyah as-Swaabuuniy (Rahimahu Allaah): Abul-´Abbaas al-Hasan bin Sufyaan an-Nasawiy ametukhabarisha: al-´Abbaas bin Subayh amewahadithia: ´Abdul-Jabbaar bin Mudhwaahir ametuhadithia: Ma´mar bin Raashid amenihadithia: Nimemsikia Ibn Shihaab az-Zuhriy akisema:

”Kufunza Sunnah ni bora kuliko kufanya ´ibaadah miaka mia mbili.”

Abu Bakr Muhammad bin ´Abdillaah bin Muhammad bin Zakariyyaa ash-Shaybaaniy ametukhabarisha: Abul-´Abbaas Muhammad bin ´Abdir-Rahmaan ad-Daghuuliy ametukhabarisha: Nimemsikia Muhammad bin Haatim al-Mudhwaffariy akisema: Nimemsikia ´Amr bin Muhammad akisema: Abu Mu´aawiyah adh-Dhwariyr alimuhadithia Haaruun ar-Rashiyd Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kuhusu mahojiano ya Aadam na Muusa (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam). Ndipo ´Iysaa bin Ja´far akasema: ”Itakuweje ilihali kuna masafa marefu kati ya Aadam na Muusa?” Haaruun akamrukia na kusema: ”Anakusimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) na wewe unampinga kwa kuuliza inakuweje?” Akaendelea kusema hivo mpaka akatulia.”

Namna hii ndivo mtu anapaswa kuyatukuza maneno yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam), nako ni kuyakabili kwa kuyakubali, kujisalimisha na kuyasadikisha. Aidha anatakiwa kumkaripia kwa ukali kila ambaye atashikamana na njia nyingine inayoenda kinyume na ya Haaruun ar-Rashiyd (Rahimahu Allaah) kwa yule ambaye anapingana na khabari Swahiyh na akayahoji kwa kuyapinga, kuona kuwa si yenye kuwezekana na asiyapokee kama ambavo anatakiwa kuyapokea yale yote yaliyotoka kwa Mtume – swalah na amani zimwendee yeye na kizazi chake!

Allaah (Subhaanah) atujaalie kuwa miongoni mwa wale tunaosikia maneno na kuyafuata yale mazuri zaidi, wenye kushikamana barabara na Qur-aan na Sunnah kipindi cha maisha yao yote na atuepushe na matamanio yenye kupotosha, maoni yenye kuharibu na shari zenye kutweza.

Mwisho wake himdi zote zote ni stahiki ya Allaah pekee. Swalah na amani zimwendee bwana wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] Abu Daawuud (4341), at-Tirmidhiy (3058) na Ibn Maajah (4014).

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 317-32
  • Imechapishwa: 02/01/2024