52. Mja ndiye mtendaji lakini Allaah ndiye mkadiriaji

Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Tunatambua kuwa Allaah (Subhaanah) hakuamrisha na kukataza isipokuwa ni mambo yanayowezekana kufanya na kuacha. Vivyo hivyo hakumtenza nguvu yeyote kufanya maasi au hakumlazimisha kuacha kitu katika utiifu. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[1]

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Basi mcheni Allaah muwezavyo.”[2]

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Leo kila nafsi italipwa kwa yale yote iliyoyachuma, hakuna dhuluma leo!”[3]

Imefahamisha kuwa mja ana khiyari ya kutenda na kuchuma, analipwa thawabu kwa wema wake na adhabu kwa uovu wake – na haya yanatendeka kwa mipango na makadirio ya Allaah.

MAELEZO

Kuoanisha kati ya kwamba kitendo cha mja kimeumbwa na Allaah na kwamba ni chumo lake.

Umekwishajua kutokana na yaliyotangulia ya kwamba kitendo cha mja kimeumbwa na Allaah na kwamba ni chumo la mja ambalo analipwa thawabu kwalo; tendo jema analipwa kwa tendo jema na tendo uvo atalipwa mfano wake. Ni vipi tutaoanisha? Namna ya kuoanisha kati yake ni kwamba tunaposema kuwa kitendo kimeumbwa na Allaah (Ta´ala) ni kutokana na mambo mawili:

1 – Kitendo cha mja ni kutokana na sifa zake. Mja na sifa zake wote wawili wameumbwa na Allaah (Ta´ala).

2 – Kitendo cha mja kinatokana na matakwa ya kimoyo na uwezo wa kimwili. Pasi na hivyo viwili asingeweza kutenda. Allaah (Ta´ala) ndiye ameweza kuumba matakwa na uwezo huu. Muumbaji wa sababu ndiye muumba wa chenye kusababishwa. Kukinasibisha kitendo cha mja kwa uumbaji wa Allaah ni kunasibisha sababu kwa yule msababishaji na si kwamba Yeye moja kwa moja ndiye amekifanya. Kwa sababu mfanyaji wa kikweli ni mja. Kwa ajili hiyo kitendo kimenasibishwa kwake kwa njia ya uchumaji na kimenasibishwa kwa Allaah kwa njia ya kukiumba na kukikadiria. Manasibisho yote mawili ni yenye kuzingatiwa. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] 02:286

[2] 64:16

[3] 40:17

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 94-95
  • Imechapishwa: 03/11/2022