Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Hatufanyi mipango na makadirio ni hoja na udhuru kwetu juu ya kuacha maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Bali ni lazima kuamini na kujua ya kwamba ni Allaah ndiye Mwenye hoja juu yetu kwa kuteremsha Vitabu na kuwatuma Mitume. Allaah (Ta´ala) amesema:

لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ

”Ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya [kuagizwa] Mitume.”[1]

MAELEZO

Matendo yote ya waja – ni mamoja yale mazuri na mabaya – yameumbwa na Allaah kama ilivyokwishatangulia. Lakini hiyo sio hoja kwa mtenda dhambi juu ya kule kufanya kwake dhambi. Hilo ni kutokana na dalili nyingi ikiwa ni pamoja na:

1 – Allaah ameegemeza kitendo cha mja Kwake na akafanya kuwa yeye ndiye amekichuma. Amesema (Ta´ala):

الْيَوْمَ تُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۚ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ

“Hii leo kila nafsi italipwa kwa yale iliyoyachuma – hakuna dhuluma leo hii!  Hakika Allaah ni Mwepesi wa kuhesabu.”[2]

Angelikuwa hafanyi kwa kutaka kwake mwenyewe na pia hana uwezo basi asingenasibishiwa.

2 – Allaah amemwamrisha na kumkataza mja na hakumlazimisha isipokuwa kile anachokiweza. Amesema (Ta´ala):

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[3]

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Basi mcheni Allaah muwezavyo.”[4]

Angelikuwa ametenzwa nguvu juu ya kufanya basi asingeweza kufanya au kujizuia. Ambaye ametenzwa nguvu hawezi kujinasua.

3 – Kila mmoja anajua tofauti kati ya kitendo anachofanya mtu kwa kutaka kwake mwenyewe au anachotenzwa nguvu. Kitendo aina ya kwanza mtu anaweza kujinasua nacho.

4 – Mtenda dhambi hajui kile alichokadiriwa kabla ya yeye kuyafanya. Isitoshe anaweza kufanya na kuacha yote mawili. Ni vipi basi atashika njia ya makosa na ajengee hoja kwa majaliwa yasiyojulikana? Je, ni vyema ashike njia ya sawa kisha aseme kuwa hayo ndio ambayo amejaaliwa?

5 – Allaah ameeleza kuwa amewatumiliza Mitume ili wasimamishe hoja:

لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ

”Ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya [kuagizwa] Mitume.”

Kama makadirio yangekuwa ni hoja kwa mtenda dhambi basi hoja isingesimama kwa kutumilizwa Mitume.

[1] 04:165

[2] 40:17

[3] 02:286

[4] 64:16

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 93-94
  • Imechapishwa: 03/11/2022