Kuamini makadiro hakukamiliki isipokuwa kwa mambo manne:

1 – Kuamini kuwa Allaah aliyajua yote yatayokuweko kwa jumla na kwa upambanuzi kwa ujuzi Wake wa awali. Amesema (Ta´ala):

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Je, hujui kwamba Allaah anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yameandikwa katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”[1]

2 – Allaah aliandika katika Ubao uliohifadhiwa makadirio ya kila kitu. Amesema (Ta´ala):

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا

 “Hakuna msiba wowote unaokusibuni katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla Hatujauumba.”[2]

Bi maana kuwaumba viumbe.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah amekadiria makadirio ya viumbe miaka 50.000 kabla ya kuziumba mbingu na ardhi.”[3]

3 – Hakupitiki kitu mbinguni na ardhini isipokuwa kwa utashi na matakwa Yake yanayozungukia kati ya rehema na hekima. Anamwongoza amtakaye kwa rehema Yake na anampotosha amtakaye kwa hekima Yake. Haulizwi kwa kile akifanyacho kutokana na ukamilifu wa hekima na ufalme Wake. Lakini wao wataulizwa. Yanayotokea katika hayo ni yenye kwenda sambamba na ujuzi Wake uliotangulia na yaliyoandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

”Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa Qadar.”[4]

وَمَن يُرِدْ أَن يُضِلَّهُ يَجْعَلْ صَدْرَهُ ضَيِّقًا حَرَجًا

”Basi yule ambaye Allaah anataka kumwongoza basi humfungulia kifua chake kwa Uislamu. Na yule ambaye anataka kumpoteza humjaalia kifua chake kuwa na dhiki chenye kubana.”[5]

Amethibitisha kuwa uongofu na upotofu vinatokea kwa kutaka Kwake.

4 – Kila kitu, mbinguni na ardhini, vimeumbwa na Allaah (Ta´ala). Hakuma Muumba asiyekuwa Yeye na wala hakuna Mola mwingine. Amesema (Ta´ala):

وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا

”Ameumba kila kitu kisha akakikadiria kipimo sawasawa.”[6]

Amesema kupitia kwa Ibraahiym:

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah amekuumbeni pamoja na vile mnavovifanya.”[7]

[1] 22:70

[2] 57:22

[3] Muslim (2653).

[4] 59:49

[5] 06:125

[6] 25:02

[7] 37:96

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 92-93
  • Imechapishwa: 03/11/2022