Isitoshe wanazuoni wana maneno mengi ambayo yanafanana na maneno ya Imaam Maalik na yana maana sawa. Kama alivyosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah):

“Isitoshe maneno ya maimamu wengine yanaenda sambamba na masimulizi ya Maalik.”[1]

Miongoni mwa maneno ya Salaf ambayo yanaenda sambamba na maneno ya Maalik ni haya yafuatayo:

1 – Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Abu Bakr al-Khallaal amepokea katika ”Kitaab-us-Sunnah” ya kuwa al-Awzaa´iy amesema:

”az-Zuhriy na Mak-huul walikuwa wakisema: ”Zipitisheni kama zilivyokuja.”

Amepokea tena kutoka kwa Waliyd bin Muslim ambaye amesema:

”Nilimuuliza al-Awzaa´iy, Maalik bin Anas na Sufyaan ath-Thawriy kuhusu Hadiyth zinazozungumzia Kuonekana na nyenginezo. Wakasema: ”Zipitisheni kama zilivyokuja pasi na kuzifanyia namna.”

Kusema kwamba zinatakiwa kuzipitisha Hadiyth kama zilivyokuja ni Radd kwa Mu´attwilah. Kusema kwamba zinatakiwa kupitishwa pasi na kufanyiwa namna ni Radd kwa Mumaththilah. az-Zuhriy na Mak-huul ndio wanafunzi wa Maswahabah wajuzi zaidi katika kipindi chao. Wale maimamu wanne waliobaki ndio walikuwa maimamu wa ulimwenguni wa wanafunzi wa wanafunzi wa Maswahabah. Hakika si vyenginevyo al-Awzaa´iy aliyataja haya baada ya kuenea Jahm ambaye alikuwa anapinga Allaah kuwa juu ya ´Arshi Yake na akipinga sifa Zake nyenginezo. Lengo ni ili watu watambue kuwa ´Aqiydah ya Salaf inaenda kinyume na hilo. Miongoni mwa tabaka lao ni Hammaad bin Zayd, Hammaad bin Salamah na wengineo.

Abul-Qaasim al-Azjiy amesimulia kuwa Mutwarrif bin ´Abdillaah amesema:

“Nimemsikia Maalik bin Anas akisema wakati anapomsikia mtu anayetupilia mbali Hadiyth za sifa: “´Umar bin ´Abdil-´Aziyz amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watawale wake waliokuja baada yake wamesunisha Shari´ah mbalimbali. Yule mwenye kuzifanyia kazi anakisadikisha Kitabu cha Allaah, anakamilisha kumtii Allaah na ni mwenye nguvu juu ya dini ya Allaah. Haifai kwa yeyote katika viumbe wa Allaah kuzibadilisha wala kuangalia chochote kinachopingana nayo. Yule mwenye kuongozwa navyo basi ndiye ameongozwa na yule mwenye kutafuta nusura kwavyo basi ndiye amenusuriwa. Na yule mwenye kwenda kinyume navyo na akafuata njia nyingine ya wasiokuwa waumini, basi Allaah atamwacha aelekee huko alikoelekea na atamchoma Motoni – na ni ubaya uliyoje wa mahali pa kuishilia!”

Kupitia cheni ya maimamu ambao wote ni waamini, al-Khallaal amepokea kutoka kwa Sufyaan bin ´Uyaynah ambaye amesema:

“Rabiy´ah bin Abiy ´Abdir-Rahmaan aliulizwa kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[2]

Amelingana juu vipi? Akajibu: “Kulingana si kitu kisichojulikana. Namna haifahamiki. Ujumbe ni wenye kutoka kwa Allaah, jukumu la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kufikisha na ni wajibu kwetu kusadikisha.”

Maneno haya pia yamepokelewa kutoka kwa Maalik bin Anas, ambaye bi mwanafunzi wa Rabiy´ah bin Abiy ´Abdir-Rahmaan.

Miongoni mwayo ni yale aliyopokea Abush-Shaykh al-Aswbahaaniy na Abu Bakr al-Bayhaqiy kupitia kwa Yahyaa bin Yahyaa ambaye amesema:

“Tulikuwa kwa Anas bin Maalik akaja bwana mmoja na akamuuliza kuhusu maneno Yake:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”

“Amelingana vipi?” Akainamisha kichwa chake kitambo kirefu mpaka akaanza kutokwa na jasho. Kisha akasema: “Kulingana ni kitu kisichojulikana. Namna haijulikani. Ni lazima kuamini hilo na ni uzushi kuuliza juu yake. Mimi sikuoni vyengine isipokuwa ni mzushi.” Kisha akaamrisha atolewe nje.”

Majibu ya Rabiy´ah na Maalik kuhusu kulingana yanaafikiana na maneno ya wengine:

”Zipitisheni kama zilivyokuja pasi na kuzifanyia namna.”

Walichokanusha ni utambuzi wa namna na si uhakika wa sifa yenyewe. Endapo watu hawa wameamini matamshi peke yake pasi na maana yake basi wasingelisema:

“Kulingana ni kitu kisichojulikana. Namna haijulikani.”

Na wala wasingelisema:

”Zipitisheni kama zilivyokuja pasi na kuzifanyia namna.”

Kwa sababu katika hali hiyo kulingana kunakuwa hakutambuliki kama mfano wa maana ya herufi zisizotambulika. Jengine ni kwamba kusingelikuwa na maana yoyote kukanusha utambuzi wa namna ikiwa haijulikani maana ya tamko. Kukanushwa kwa ujuzi wa namna kunakuwa muhimu pale ambapo kunathibitishwa sifa.

Isitoshe ambaye anapinga sifa hahitaji kusema ”pasi na kuzifanyia namna”. Anayesema kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hayuko juu ya ´Arshi hana haja ya kusema ”pasi na kumfanyia namna”. Hivyo basi, ingelikuwa ´Aqiydah ya Salaf ni kukanusha sifa basi wasingelisema ”pasi na kumfanyia namna”.

Pamoja na maneno yao ”Zipitisheni kama zilivyokuja pasi na kuzifanyia namna” yanapelekea majulisho ya Hadiyth kubaki kama zilivyo. Kwani yanafahamisha maana. Ingelikuwa majulisho ya Hadiyth ni yenye kukanushwa basi ingelipaswa kusema:

”Yapitisheni matamshi yake pasi na kuamini ule uinje wake.”

au:

”Yapitisheni matamshi yake pasi na kuamini kuwa Allaah hasifiwi kwa njia hiyo.”

Katika hali hiyo hayawi yamepitishwa kama yalivyokuja na hivyo basi kusingelisemwa ”pasi na kuzifanyia namna”. Kwa sababu ni upuuzi kukanusha namna ya kitu ambacho hakikuthibiti.

al-Athraam, Ibn Battwah, Abu ´Umar at-Twalamankiy na wengineo wamepokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa ´Abdul-´Aziyz bin Abiy Salamah al-Maajashuun – ambaye ni mmoja katika wale maimamu watatu wa Madiynah pamoja na Maalik bin Anas na Ibn Abiy Dhi’b – kwamba aliulizwa juu ya yale yaliyokanushwa na Jahmiyyah:

“Nimefahamu kuwa unauliza kuhusu yale ambayo Jahmiyyah na wale wapinzani wao wanaonelea kuhusu sifa za Mola Mtukufu ambaye utukufu Wake unapita maelezo na makadirio. Ndimi zinashindwa kufasiri sifa Zake na akili zinashindwa kuelewa uwezo Wake. Ukuu Wake umekataliwa na akili na haikupata njia isipokuwa kurudi hali ya kuwa imehizika, imenyong’onyea. Hakuna kingine walichoamrishwa isipokuwa kutazama na kutafakari katika yale Aliyoumba kwa ukamilifu wake. Swali “Vipi?” huulizwa kwa kitu ambacho hakikuwepo kisha baadaye kikawepo. Kuhusu Yule ambaye habadiliki wala hapotei na wala hakuna mfano Wake hakuna anayejua namna alivyo isipokuwa Yeye tu. Ni vipi atajulikana kiwango Chake Yule ambaye hakuzaliwa, hafi na wala hateketei? Ni vipi sifa Zake zitaambatanishwa na mpaka na mwisho? Mtambuzi ndiye anamjua na msifiaji ndiye anathibitisha kiwango Chake juu ya kwamba Yeye ni wa Haki ilio wazi – hakuna haki ambayo ni haki zaidi kuliko Yeye, hakuna chochote ambacho kiko wazi zaidi kuliko Yeye. Dalili ya kwamba akili haiwezi kuelewa sifa Zake ni kwamba haiwezi hata kuzielewa sifa za viumbe vilivyo vidogo zaidi; ni ndogo sana kiasi cha kwamba zinakaribia kutoziona. Zinabadilika na kupotea wala hakuonekani masikizi wala maono yao. Kwa sababu yale wanayoyafanya na kuyadhania yamejificha zaidi kwako kuliko yale yanayodhihiri katika masikizi na maono yao. Amebarikika Allaah, mbora wa waumbaji, Muumbaji wao, Bwana wa mabwana wao na Mola wao:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.”[3]

Allaah akulinde kutokana na kupekua sifa ambayo Allaah hakujisifu nayo Mwenyewe, kwa sababu huwezi kumkadiria yale aliyojisifu Mwenyewe. Ikiwa huwezi kumkadiria yale aliyojisifu Mwenyewe, ni vipi basi unaweza kupekua yale ambayo hakujisifu? Utafanya hayo kwa ajili ya kumtii au utaepuka kitu katika yale aliyoyakataza.. Yale ambayo Allaah amejisifu Mwenyewe na kupitia kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi na sisi tutamsifu kama alivyojisifu Mwenyewe na wala hatotojikakama sifa yoyote ambayo Yeye hakuitaja.”[4]

[1] Sharh Hadiyth-in-Nuzuul, uk. 34.

[2] 20:05

[3] 42:11

[4] al-Hamawiyyah, uk. 24-27.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 72-74
  • Imechapishwa: 15/12/2025