Anapaswa afanye kisomo chake kwa utulivu na kwa mpangilio mzuri. Wanazuoni wote wamekubaliana juu ya kupendekezwa kufanya kisomo kwa utulivu na kwa mpangilio mzuri. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا

“… soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu na utungo.”[1]

Vilevile imethibiti kutoka kwa Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba alielezea kwamba:

”Kisomo cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kilikuwa ni usomaji uliofafanuliwa herufi kwa herufi.”[2]

Ameipokea Abu Daawuud, an-Nasaaiy na at-Tirmidhiy, ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.

Mu´aawiyah bin Qurrah ameeleza ya kwamba ´Abdullaah bin Mughaffal (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesema:

”Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya kufunguliwa kwa mji wa Makkah akiwa juu ya ngamia wake akisoma Suurah al-Fath, akirudia kuipamba sauti yake katika usomaji wake.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Kusoma Suurah moja kwa utaratibu na ipasavyo ni bora zaidi kwangu kuliko kusoma Qur-aan yote.”

Mujaahid aliulizwa kuhusu watu wawili ambapo mmoja amesoma ”al-Baqarah” na ”Aal ´Imraan” na mwingine amesoma ”al-Baqarah” pekee, lakini muda wao wa kusoma, Rukuu´, sujuud na ukaaji wao ni sawa. Akajibu:

”Yule aliyesoma al-Baqarah pekee ndiye bora zaidi.”

Imekatazwa kufanya haraka kupita kiasi katika kusoma Qur-aan, jambo ambalo huitwa kukimbiza sana kisomo. Imethibiti ya kwamba bwana mmoja alimwambia ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh):

“Mimi nasoma Mufasswal zote katika Rak´ah moja.” Ndipo Ibn Mas´uud akamwambia: “Hivi hivi kama mashairi? Hakika kuna watu wanaisoma Qur-aan lakini haivuki koo zao. Lakini inapopenya moyoni na kukaa humo ndipo inaleta manufaa.”[4]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim, ambaye tamko ni lake.

Wanazuoni wamesema kwamba kusoma Qur-aan kwa utaratibu na ipasavyo ni jambo linalopendeza kwa ajili ya kutafakari na kwa sababu nyinginezo. Aidha kusoma kwa utaratibu na ipasavyo ni jambo linalopendeza kwa asiye mwarabu ambaye haelewi maana yake, kwa sababu hilo linakaribisha zaidi heshima na utukufu wa Qur-aan na pia lina athari kubwa zaidi katika moyo.

[1] 73:4

[2] Abu Daawuud (1466) na at-Tirmidhiy (2923), aliyesema kuwa Hadiyth ni nzuri, Swahiyh na ngeni. Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan Abiy Daawuud” (1466).

[3] al-Bukhaariy (4281, 4835, 5034, 5047 na 7540) na Muslim (794).

[4] al-Bukhaariy (775, 4996 na 5043) na Muslim (822).

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 57-59
  • Imechapishwa: 02/09/2026