Imepita katika vipengele viwili vilivyotangulia maelezo ya yale yanayosababisha kulia wakati wa kusoma na hiyo ni sifa ya wanaomjua Allaah na ni alama ya waja wema wa Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَيَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ يَبْكُونَ وَيَزِيدُهُمْ خُشُوعًا

”Wanaporomoka kifudifudi hali ya kulia na inawazidishia unyenyekevu.”[1]

Kumepokelewa Hadiyth nyingi pamoja na masimulizi ya Salaf kuhusu jambo hilo. Miongoni mwa hayo ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Someni Qur-aan na lieni. Msipolia basi jilazimisheni kulia.”[2]

´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) aliswalisha watu swalah ya Fajr na akasoma Suurah ”Yuusuf”, ambapo akalia mpaka machozi yake yakatiririka mpaka kwenye kifua chake. Imekuja katika upokezi mwingine ya kwamba ilikuwa katika swalah ya ´Ishaa, jambo linalofahamisha ya kuwa kitendo hicho kilikariri kwake. Imekuja katika upokezi mwingine ya kwamba alilia mpaka watu wakasikia kilio chake kutoka nyuma ya safu.

Abu Rajaa´ amesema:

”Nilimwona Ibn ´Abbaas ambaye chini ya macho yake kulikuwa kama alama zilizochoka kutokana na wingi wa kulia.”

Abu Swaalih amesema:

”Kundi la watu kutoka Yemen walikuja kwa Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo wakaanza kusoma Qur-aan na kulia. Ndipo Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) akasema: ”Hivi ndivyo tulivyokuwa.”

Hishaam amesema:

”Wakati mwingine ilikuwa inaweza kutokea nikasikia kilio cha Muhammad bin Siyriyn usiku akiwa ndani ya swalah.”

Masimulizi juu ya mada hii ni mengi na hatuwezi kuyadhibiti, lakini tuliyoyataja na kuyaashiria yanatosha – na Allaah ndiye Mjuzi zaidi. Imaam Abu Haamid al-Ghazaaliy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Kulia kunapendekezwa wakati wa kisomo na wakati mwingine… Njia ya kukipata ni mtu kuleta huzuni moyoni mwake kwa kutafakari vitisho, adhabu kali, ahadi na maagano yaliyomo ndani yake, kisha atafakari upungufu wake katika hayo. Ikiwa hatapata huzuni na kulia, kama wanavyopata watu maalum, basi na alie kwa kukosa hali hiyo. Kwa sababu hilo ni katika misiba mikubwa zaidi.”

[1] 17:109

[2] Ibn Maajah (1337 och 4196). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan Ibn Maajah” (250).

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 56-57
  • Imechapishwa: 02/09/2026