Swali 51: Je, swalah ya mkusanyiko inawahiwa kwa kuwahi kutoa Tasliym pamoja na imamu au inawahiwa kwa kuwahi Rak´ah moja? Kukiingia kikosi cha waswaliji na kumkuta imamu yuko katika Tashahhud ya mwisho – je, bora ni wao kujiunga pamoja na imamu au wasubiri atoe salamu na waswali mkusanyiko wao?

Jibu: Swalah ya mkusanyiko haiwahiwi isipokuwa kwa kuwahi Rak´ah. Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayewahi Rak´ah ya swalah, basi ameiwahi swalah.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Lakini ambaye alikuwa na udhuru unaokubalika katika Shari´ah basi anapata fadhilah za swalah ya mkusanyiko ijapo hakuwahi kuswali na imamu. Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi mja anapokuwa mgonjwa au akasfiri, basi Allaah humwandikia yale aliyokuwa akiyafanya hali ya kuwa mzima na mkazi.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake.

Vilevile amesema (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Tabuuk:

“Hakika Madiynah wako watu ambao hakumpita masafa yoyote wala hamkuvuka bonde lolote isipokuwa wako pamoja nanyi. Kilichowazuia ni udhuru.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Hakika Madiynah wako watu ambao hamkupita masafa yoyote wala hamkuvuka bonde lolote isipokuwa wameshirikiana nanyi katika ujira. Kilichowazuia ni udhuru.”

Kuna maafikiano juu yake.

Watu hawa ambao wamemkuta imamu katika Tashahhud ya mwisho kujiunga naye ndio bora. Hilo ni kutokana na ueneaji wa maneno yake (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam):

“Mtapoijilia swalah basi tembeeni na lazimianeni na utulivu. Kile mtachowahi kiswalini na kile kitachokupiteni kikamilisheni.”

Kuna maafikiano yake.

Endapo wataswali mkusanyiko kivyao hapana neno – Allaah akitaka.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 56-57
  • Imechapishwa: 05/09/2022