Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Ilipokuwa jambo lao limeegemezwa juu ya misingi hii miwili ya kikafiri na ya uwongo ndipo ikapelekea kuwatia ujingani wale wanamme wa mwanzo waliotangulia na kuwaona kuwa si wasomi. Wanawazingatia kuwa ni wema wa kawaida ambao hawana utambuzi uliobobea kuhusu Allaah na utambuzi wa kiungu. Ukiongezea ya kwamba watukufu waliokuja nyuma  wako na utambuzi huo.

MAELEZO

Kwa sababu wameijenga ´Aqiydah yao juu ya misingi miwili:

1 – Salaf hawaifahamu Qur-aan na kwamba wale waliokuja baadaye ndio wanaifahamu.

2 – Dalili za Qur-aan na Sunnah ni za kutia dhana tu ilihali dalili za mantiki ni za kukata kabisa.

´Aqiydah hii ndio matokeo ya misingi hii miwili ambayo inatokana na kuwatuhumu ujinga Salaf, waghafilikaji na kuwafanya ni wema wa kawaida na kuona kuwa wale waliokuja nyuma ndio wajuzi na ndio wenye kutangulizwa mbele katika elimu. Matokeo yake wakasema kuwa Salaf walikuwa wajinga na watu wasiokuwa wasomi ambao walikuwa wakihifadhi tu pasi na kufahamu.

Kwa mujibu wa watu hawa Salaf walikuwa wajinga kwa sababu hawakubobea katika mantiki na mijadala. Wakimaanisha kuwa Maswahabah na wanafunzi wa Maswahabah walikuwa kama watu wa kawaida tu ambao hawakuwa na jengine zaidi ya kuhifadhi tu Qur-aan na Sunnah pasi na kuzifahamu. Sambamba na hilo wale waliokuja nyuma walifahamu kinachokusudiwa kwa maandiko. Kwa ajili hiyo, wanadai, wao ni wajuzi zaidi kuliko Salaf. Upande wa pili wanadai kuwa mfumo wa Salaf umesalimika zaidi kwa sababu hawakuingia ndani ya tafsiri bali walitegemeza maana yake kwa Allaah. Huu ni mgongano. Kwa sababu salama haipatikani pasi na elimu. Hakuna salama yoyote kunapokuwa ujinga.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 12/08/2024