50. Radd kwa mwenye kudai kwamba du´aa sio ´ibaadah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mlango wa nane

Radd kwa mwenye kudai kwamba du´aa sio ´ibaadah

Akisema: “Mimi siabudu mwengine yeyote isipokuwa Allaah, na huku kutafuta kinga kwa watu wema na kuwaomba [du´aa] sio ´ibaadah”. Mwambie: “Wewe unakubaliana na mimi ya kwamba Allaah kafaradhisha juu yako kumtakasia ´ibaadah, na ni haki Yake juu yako?”

Akisema: “Ndio”, mwambie: “Nibainishie hili ulilofaradhishiwa juu yako, ambalo ni kumtakasia ´ibaadah Allaah pekee, na ni haki Yake juu yako!” Ikiwa hajui ´ibaadah ni nini na aina zake, mbainishie hayo kwa kile anachosema Allaah (Ta´ala):

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

“Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye hapendi wavukao mipaka.” (07:55)

Ukishamjuza haya, mwambie: “Umejua sasa kuwa haya [unayofanya] ni ´ibaadah?” Hana budi kusema: “Ndio” – na du´aa ndio kilele cha ´ibaadah.

MAELEZO

Mtu huyo akisema kuwa yeye hawaabudu kama anavyomuabudu Allaah (´Azza wa Jall) na kwamba kuwaelekea na kuwaomba [du´aa] sio ´ibaadah, hii ni hoja tata. Mwambie kuwa Allaah amekufaradhishia kumtakasia ´ibaadah Yeye pekee. Akikubaliana na wewe, muulize ni nini maana ya kumtakasia ´ibaadah. Ima atakuwa ni mwenye kujua au hajui. Ikiwa hajui, basi mbainishie ili ajue kuwa kuwaomba watu wema na kuwaelekea ni ´ibaadah.

Mbainishie aina mbalimbali za ´ibaadah na mwambie kuwa Allaah anasema:

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

“Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye hapendi wavukao mipaka.”

Du´aa ni ´ibaadah. Mambo yakishakuwa ni namna hii, kumuomba asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall) ni shirki. Kujengea juu ya hili, yule ambaye anastahiki kuombwa, kuabudiwa na kutarajiwa ni Allaah peke Yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 66
  • Imechapishwa: 24/11/2023