50. Dalili inayofahamisha uola wa Allaah na kustahiki Kwake kuabudiwa II

Maneno yake:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ

”Na katika alama Zake ni usiku na mchana, jua na mwezi. Hivyo basi msisujudie jua na wala mwezi, bali msujudieni Allaah ambaye Aliyeviumba – ikiwa Yeye pekee ndiye mnamwabudu.”[1]

Bi maana miongoni mwa alama Zake zinazofahamisha juu ya uola, uwezo na kustahiki Kwake ´ibaadah pasi na mwengine ni usiku unaotia giza na mchana ambao unaangaza ulimwengu mzima. Hizi ni miongoni mwa maajabu ya alama za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Ni nani ambaye anaufanya ulimwengu mzima kuingiwa na giza katika mkupuko mmoja kisha anaufanya ulimwengu mzima kuangaza katika mkupuko mmoja? Ni Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Lau watakusanyika viumbe ili kuangaza maeneo fulani ardhi basi hawatoweza kufanya hivo isipokuwa maeneo madogo sana yenye ukomo. Endapo wataleta mashine za umeme zilizoko dunia nzima hazitoangaza isipokuwa maeneo fulani yenye ukomo ardhini. Kuhusu jua na mwezi vinaangaza ulimwengu mzima. Mchana na usiku vinapatikana vivyo hivyo jua na mwezi. Amesema (Ta´ala):

لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ

“Hivyo basi msisujudie jua na wala mwezi, bali msujudieni Allaah ambaye Aliyeviumba – ikiwa Yeye pekee ndiye mnamwabudu.”

Hapa kunabatilishwa shirki. Usiwasujudie viumbe. Kwa sababu miongoni mwa viumbe vikubwa ni jua na mwezi. Jengine ni kwamba washirikina walikuwa wakiabudu mwezi na wakilisujudia. Miongoni mwao wako waliokuwa wakiabudu mwezi na nyota, kama mfano wa watu wa Ibraahiym. Walikuwa wakiyajengea mahekalu kwa miundo ya nyota na wakiviabudu. Ndipo akasema (Ta´ala):

لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ

“Hivyo basi msisujudie jua.”

Kusujudu maana yake ni kuweka paji la uso juu ya ardhi hali ya kumnyenyekea yule unayemwabudu. Hii ndio aina kubwa kabisa ya ´ibaadah. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Karibu zaidi anapokuwa mja kwa Mola Wake ni pale aliposujudu.”[2]

Aina kubwa zaidi ya ´ibaadah ni kusujudu kwako juu ya ardhi. Kwa sababu uso wako ambao ndio kitu kitukufu zaidi kwako umeunyenyekeza kwa Allaah juu ya ardhi hali ya kumwabudu Allaah na kujidhalilisha mbele Yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Hii ndio Sujuud ya kihakika. Haistahiki kumfanyia hivo mwengine asiyekuwa Allaah. Lakini kulisujudia jua na mwezi ni kusujudia viumbe visivyostahiki kufanyiwa hivo. Haijuzu kuwasujudia viumbe. Anayetakiwa kusujudiwa ni Muumba wa viumbe. Kuhusu viumbe ni viumbe mfano wako wanaoendeshwa. Inakuweje unawasujudia viumbe wasiokuwa na uwezo mfano wako? Kitendo hichi hakifai. Akili yako imeenda wapi?

 Muumbaji (Subhaanahu wa Ta´ala) ambaye hashindwi na kitu ndiye anastahiki kusujudiwa. Sujuud ni haki ya Allaah (´Azza wa Jall). Sio haki ya viumbe vovyote watavyokuwa. Kiumbe huyu, pamoja na ukubwa na majivunao yake, yeye bado ni kiumbe mnyonge tena anayeendeshwa:

لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ

“Hivyo basi msisujudie jua na wala mwezi, bali msujudieni Allaah ambaye Aliyeviumba – ikiwa Yeye pekee ndiye mnamwabudu.”

Kilicho cha wajibu ni kutomwabudu mwengine asiyekuwa Allaah pekee. Mkimsujudia Yeye na wakati huohuo mkawasujudia wengine mtakuwa sio wenye kumwabudu Allaah ´ibaadah sahihi. Bali mtakuwa ni wenye kumwabudu pamoja na shirki, kitu ambacho kinaiharibu ´ibaadah.

[1] 41:37

[2] Muslim (482).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 109-111
  • Imechapishwa: 17/12/2020