49. Ni kina nani kundi lililookoka na kundi lililonusuriwa katika hii leo?

Swali 49: Ni kina nani kundi lililookoka na kundi lililonusuriwa katika hii leo? Ni zipi sifa zake?

Jibu: Kundi lililookoka na kundi lililonusuriwa hii leo mpaka siku ya Qiyaamah ni lile ambalo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

”Mayahudi wamegawanyika makundi sabini na moja. Manaswara wamegawanyika makundi sabini na mbili.  Na ummah wangu utagawanyika katika mapote sabini na mbili. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: ”Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Ni lile linalofuata yale ninayofuata mii hii leo na Maswahabah zangu.”

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema juu yao:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia mwanzoni ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[1]

Miongoni mwa sifa za kundi hilo ni kwamba ni wenye kushikamana barabara ni yale aliyokuwemo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake.

Sifa yao nyingine ni kuwa ni wenye kusubiri juu ya haki na wala hawazingatii fikira za wale wanaokwenda kinyume. Hawajali kwa ajili ya Allaah lawama za wenye kulaumu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hatokuacha kuwepo kikundi kutoka katika ummah wangu hali ya kuwa ni chenye kushinda juu ya haki. Hakitodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura wala wale wenye kwenda kinyume nao mpaka ifike amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) wakiwa katika hali hiyo.”[2]

Sifa yao nyingine ni kuwa wanawapenda Salaf, wanawasifu, wanawaombea du´aa na kushikaamana na mapokezi yao.

Moja ya sifa yao nyingine ni kuwa hawamchukii yeyote katika Salaf, ni mamoja ni Maswahabah au wale waliokuja baada yao[3].

Miongoni mwa alama za mapote yaliyopinda ni kuwa wanawachukia Salaf na wanachukia mfumo wa Salaf na kutahadharisha nao[4].

[1] 09:100

[2] Muslim (1920).

[3] Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin ´Aliy al-Barbahaariy amesema:

”Ukimuona mtu anampenda Abu Hurayrah, Anas bin Maalik, Usayd bin Hudhwayr, basi tambua kuwa ni mtu wa Sunnah – Allaah akitaka.

Ukimuona mtu anampenda Ayyuub, Ibn ´Awn, Yuunus bin ´Ubayd, ´Abdullaah bin Idriys al-Awdiy, ash-Sha´biy, Maalik bin Mighwal, Yaziyd bin Zuray´, Mu´aadh bin Mu´aadh, Wahb bin Jariyr, Hammaad bin Salamah, Hammaad bin Zayd, Maalik bin Anas, al-Awzaa´iy na Zaaidah bin Qudaamah, basi jua kuwa ni mtu wa Sunnah.

Ukimuona mtu anampenda Ahmad bin Hanbal, al-Hajjaaj bin Minhaal na Ahmad bin Naswr, akawataja kwa uzuri na akafuata maoni yao, basi tambua kuwa ni mtu wa Sunnah.” (Sharh-us-Sunnah, uk. 120-121)

[4] al-Barbahaariy amesema:

”Ukimuona mtu anamtukana yoyote katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi elewa kuwa ni mtu mwenye maoni maovu na ni mtu mwenye kufuata matamanio yake.” (Sharh-us-Sunnah, uk. 115)

Amesema tena:

”Ukimsikia mtu anayatukana au kuyarudisha mapokezi au anatamani kitu kingine mbali na mapokezi, basi utuhumu Uislamu wake na usishuku kuwa ni mtu mwenye kufuata matamanio na mzushi.” (Sharh-us-Sunnah, uk. 115-116)

Qutaybah bin Sa´iyd amesema:

”Ukimuona mtu anawapenda Ahl-ul-Hadiyth, basi tambua kuwa anafuata Sunnah. Anayekwenda kinyume na haya basi tambua kuwa ni mzushi.” (Shi´aar Awshaab-il-Hadiyth, uk. 7)

Abu Haatim ar-Raaziy amesema:

”Alama ya Ahl-ul-Bid´ah ni kuwatukana Ahl-ul-Athar.” (al-Laalakaa’iy (1/179))

Taarifa zaidi tazama ”Lamm-ud-Durr” na mlango unaozungumzia alama za Ahl-us-Sunnah na alama za Ahl-ul-Bid´ah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 136
  • Imechapishwa: 04/03/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy