49. Ndani ya Qur-aan na Sunnah kuna mifumo inayotosheleza

Shaykh Bakr bin ´Abdillaah Abu Zayd (Rahimahu Allaah) amesema:

“Miongoni mwa rehema za Allaah (Ta´ala) kwa waja Wake na upeo wa mwisho wa hekima Yake katika Shari´ah Yake katika yale ambayo kwayo anawatengeneza waja na miji, ni pamoja na kuweka Shari´ah ya jihaad, kujitetea, kuamrisha yaliyo mema, kukemea maovu, nasaha na ulinganizi. Kwa mfano ameweka jihaad ya nafsi, jihaad ya mali, jihaad ya silaha, jihaad ya kujitetea na kadhalika. Mfano mwingine ni kubadilisha maovu kwa kutumia mkono, jambo ambalo linarejea kwa mamlaka, wakiwemo maafisa wa polisi, na kubadilisha maovu kwa mdomo, kwa kalamu na kwa moyo. Vivyo hivyo kuamrisha mema. Njia bora ya kuwatakia mema viongozi wa waislamu na watu wa kawaida ni kwa kuwanasihi kwa mdomo na kuwanasihi kwa kuwaandikia na kuwakumbusha kuhusu Qiyaamah.

Ulinganizi unatakiwa uwe kwa kazi zilizopangwa ndani ya Uislamu, kama vile Khutbah za ijumaa, Khutbah za ´iyd, hajj, mafunzo na vikao vya elimu. Mtu asimamie haki kwa kuibainisha mpaka aweze kuondosha hali yenye kuhuzunisha ya Ummah. Kwa fatwa ya mwanachuoni anayezingatiwa Allaah huzibadilisha hali za watu kwenda katika hali bora zaidi. Fatwa kama hiyo inafanya makubwa zaidi kuliko yanayofanywa na makundi na mapote. Vivyo hivyo kitendo cha mwanachuoni mmojammoja; anaeneza elimu yake katika Ummah; katika eneo, jimbo, mji, kijiji na kadhalika. Kadhalika kwa kitendo cha pamoja kwa mujibu wa mfumo wa kinabii – na si kwa mfumo mwingine – kama vile maafisa wa polisi wa kidini, vituo vya ulinganizi na miungano ya wanazuoni.”[1]

Mifumo hii yenye kuenea iliyowekwa katika Shari´ah iko katika kilele cha mwisho cha uwazi kwa ambaye anazingatia Qur-aan na Sunnah na wasifu wa Salaf. Ni makafiri wangapi walisilimu kupitia njia hizo! Ni watenda madhambi wangapi walitubu kupitia njia hizo! Ni wapotofu wangapi wameongoka kupitia njia hizo! Ni wangapi waliokosea wamepata mwongozo kupitia njia hizo!

[1] Hukm-ul-Intimaa’, uk. 157-158

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 68-69
  • Imechapishwa: 24/05/2023