Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema pia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni:

“… kiongozi wa Mitume… “

Yeye Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kiongozi wa wana wa Aadam, kama alivosema mwenyewe:

“Mimi ni kiongozi wa wana Aadam na si fakhari.”[1]

Amewaeleza Ummah kitu hicho kwa minajili ya kumshukuru Allaah (´Azza wa Jall) na ili Ummah wake wamshukuru Mola Wake juu ya neema hii kumfanya Mtume wake ndio bwana wa Mitume. Bwana maana yake ni mtangulizi na kiongozi. Kwa hiyo yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye Mtume bora na kiongozi na mtangulizi wao.

Mtunzi amesema:

“… na kipenzi wa Mola wa walimwengu.”

Tamko hili ni lenye kukosolewa. Kwa sababu haitoshi kusema kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kipenzi wa Allaah (حبيب) bali kipenzi wa hali ya juu (خليل). Mapenzi ya hali ya juu ni ngazi ya juu zaidi kuliko mapenzi yaliyoachiwa. Kuna aina nyingi ya mapenzi na ngazi ya juu zaidi ni mapenzi ya hali ya juu ambayo ni yale mapenzi safi kabisa. Viumbe wawili pekee ndio wamepata ngazi hii: Ibraahiym (´alayhis-Salaam):

وَاتَّخَذَ اللَّـهُ إِبْرَاهِيمَ خَلِيلًا

“Allaah amemfanya Ibraahiym kuwa ni kipenzi wa karibu.”[2]

na Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Hakika Allaah amenifanya kuwa kipenzi Wake wa hali ya juu kama alivyomfanya Ibraahiym kuwa kipenzi Wake wa hali ya juu.”[3]

Kwa hivyo haitakiwi kusema mpenzi wa Allaah kwa sababu hayo yanaweza kusemwa kwa kila muumini na hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakuwa hatofautiani na wengine. Lakini mapenzi ya hali ya juu hachangii na wengine wote.

[1] Muslim (2278).

[2] 4:125

[3] Muslim (532).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 09/12/2022