49. Kuswali swalah ya mkusanyiko ya pili baada ya kumalizika ya kwanza

Swali 49: Baadhi wamesema kuwa haijuzu kusimamisha swalah ya mkusanyiko ya pili msikitini baada ya kumalizika mkusanyiko wa waswaliji. Je, kitu hiki kina msingi? Ni yepi ya sawa?

Jibu: Maneno haya si sahihi na wala hayana msingi wowote katika Shari´ah takasifu kutokana na ninavojua. Bali Sunnah Swahiyh inajulisha kinyume chake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalah ya mkusanyiko ni bora kuliko swalah ya anayeswali peke yake kwa ngazi ishirini na saba.”

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalah ya mwanamme na mwanamme mwingine ni takasifu zaidi kuliko swalah yake mwenyewe.”

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipomuona bwana mmoja ameingia msikitini baada ya watu kumaliza kuswali:

”Ni nani atakayemtendea wema huyu akaswali pamoja naye”?

Lakini haijuzu kwa muislamu kujichelewesha na swalah ya mkusanyiko. Bali ni lazima kwake kuharakisha wakati anaposikia adhaana.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 55
  • Imechapishwa: 05/09/2022