Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

79 – Sisi tunayaamini yote hayo.

80 – Hatufarikishi kati ya yeyote katika Mitume Wake. Tunawasadikisha wote kwa yale waliyokuja nayo.

81 – Watenda madhambi makubwa [wa ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)][1] hawatodumishwa Motoni milele pale watapokufa hali ya kuwa ni wapwekeshaji. Ikiwa hawakutubu, muda wa kuwa watakutana na Allaah hali ya kuwa ni wenye kutambua [na wenye kuamini][2]. Atawahukumu vile anavyotaka. Akitaka atawasamehe na kuwasalimisha kutokana na fadhilah Zake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema katika Kitabu Chake:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa, lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[3]

MAELEZO

Bi maana dhambi zisizokuwa shirki, kwa maana nyingine kufuru. Hakuna tofauti kati ya hayo mawili upande wa ki-Shari´ah. Kila kufuru ni shirki na kila shirki ni kufuru, kama inavofahamisha mazungumzo kati ya yule muumini mwenye bustani ya mizabibu na yule kafiri mwenye bustani ya mizabibu waliyotajwa katika Suurah ”al-Kahf”. Yazingatie hayo, hivyo utaondokewa na mambo mengine yenye kutatiza.

[1] Yaliyoko ndani ya mabano hayapatikani katika zile hati tatu za mkono wala ndani ya machapisho. Sahihi zaidi ni kuyaondosha, kwa sababu yanaashiria maana ya kwamba watenda madhambi makubwa katika nyumati zingine, kabla ya kufutwa Shari´ah hizo, hukumu yao inatofautiana na watenda madhambi makubwa ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), jambo ambalo linahitaji kuangaliwa vyema. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtoeni Motoni yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na dinari, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na nusu dinari, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na kokwa ya tende, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na dudu mchungu na halafu yule ambaye yuko na imani ya chini chini chini kabisa kuliko dudu mchugu.” (al-Bukhaariy (7510) na Muslim (193))

Hakufanya maalum ummah wake juu ya jambo hilo, bali ametaja imani kwa njia ya kuachia, hivyo basi zingatia jambo hilo.

Jengine ni kwamba wametofautiana katika kutambulisha ni ipi dhambi kubwa. Utambulisho bora ni ule unaosema kuwa dhambi kubwa ni ile ambayo inapelekea kuadhibiwa au akatishiwa kuingizwa Motoni, kulaaniwa au ghadhabu. Rejea ”Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah” ya Ibn Abiyl-´Izz na “Majmuu´-ul-Fataawaa” (11/650) ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah.

[2] Yaliyoko kati ya mabano ni ziada kutoka kwenye nakala tatu zingine. Ni ziada muhimu inayokosekana katika baadhi ya ziada, ikiwemo nakala ya Ibn Abiy-´Izz, ambaye amesema:

”Ingelikuwa vyema  na bora zaidi kusema ”waumini” badala ya ”wenye kutambua”, kwa sababu ambaye anamjua Allaah na asimwamini ni kafiri. Ambaye ametosheka na utambuzi peke yake ni al-Jahm, na ´Aqiydah yake ni yenye kurudishwa na ya batili.”  (Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 527)

[3] 4:48

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 72-73
  • Imechapishwa: 07/10/2024