Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Waumini watamuona Mola Wao Aakhirah kwa macho yao. Watamtembelea, atazungumza nao na wao watazungumza Naye. Allaah (Ta´ala) amesema:

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌإِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

”Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.”[1]

Amesema (Ta´ala):

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ

“Hapana! Hakika wao siku hiyo watawekewa kizuizi [wasimuone] Mola wao.”[2]

Pindi alipowazuia watu hao katika hali ya kuwakasirikia nao, basi ikafahamisha ya kwamba waumini watamuona katika hali ya Yeye kuridhika. Vinginevyo kusingelikuwa tofauti kati yao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kwa hakika nyinyi mtamuona Mola Wenu kama mnavyoona mwezi huu – hamtosongamana katika kumtazama.”[3]

Hadiyth ni Swahiyh iliopokelewa na al-Bukhaariy na Muslim.

Ushabihisho huu ni ushabihisho wa maono, na si kwa kitachoonwa, kwa hakika Allaah (Ta´ala) hana anayefanana Naye wala mwenza.

MAELEZO

Haiwezekani kabisa kumuona Allaah duniani. Allaah (Ta´ala) alimwambia Muusa baada ya kumuomba kumuona:

لَن تَرَانِي

”Hutoniona!”[4]

Allaah kuonekana Aakhirah ni jambo limethibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Allaah (Ta´ala) amesema:

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌإِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

”Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.”[5]

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ

“Hapana! Hakika wao siku hiyo watawekewa kizuizi [wasimuone] Mola wao.”[6]

Wakati walipozuiwa waovu kumuona ikafahamisha kuwa wema watamuona. Vinginevyo kusingelikuwa na tofauti kati yao.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kwa hakika nyinyi mtamuona Mola Wenu kama mnavyoona mwezi huu – hamtosongamana katika kumtazama.”

Kuna maafikiano juu yake.

Ushabihisho huu ni ushabihisho wa maono, na si kwa kitachoonwa, kwa hakika Allaah (Ta´ala) hana anayefanana Naye wala mwenza.

Salaf wameafikiana juu ya kuwa waumini watamuona Allaah (Ta´ala) pasi na makafiri kwa dalili ya Aayah mbili zilizotangulia. Watamuona katika uwanja wa Qiyaamah na baada ya kuingia Peponi kwa namna anayotaka (Ta´ala). Ni kuonekana kikweli kunakolingana na Allaah.

Ahl-ut-Ta´twiyl wamefasiri eti kinachokusudiwa ni kuona thawabu za Allaah au kwamba kinachokusudiwa ni kuona kwa njia ya ujuzi na kuwa na yakini. Tunawaraddi kutokana na tafsiri yao ya kwanza kwa yale yaliyokwishatangulia katika kanuni ya nne na kutokana na tafsiri yao ya pili kwa kanuni hiyohiyo. Kuna njia nyingine ya nne ya kwamba ujuzi na yakini ni mambo hutokea kwa wema hapa duniani na isitoshe ni mambo yatayotokea kwa waovu huko Aakhirah[7].

[1] 75:22–23

[2] 83:15

[3] al-Bukhaariy (554) na (574) na Muslim (633).

Hadiyth za kuhusu Allaah kuonekana Aakhirah zimepokelewa kwa mapokezi mengi (متواترة). Hayo yametajwa na wanazuoni wengi akiwemo Ibn-ul-Qayyim katika ”Haadiy Arwaah”, uk. 277, Ibn Abiyl-´Izziy katika ”Sharh-ut-Twahaawiyyah” (01/215) na Haafidhw Ibn Hajar katika ”Fath-ul-Baariy” (01/203).

Rejea katika yale yaliyoandikwa juu ya suala hili kama vile ”Taswdiyq bin-Nadhwari ilaa Allaah (Ta´ala) fiyl-Aakhirah” ya al-Aajurriy na ”Dhway´ as-Saariy ilaa Ma´rifati Ru´yat-il-Baariy” ya Abu Shaamah al-Maqdisiy na vyote viwili vimekwishachapishwa.

[4] 07:143

[5] 75:22–23

[6] 83:15

[7] Rejea walipojibiwa wale wanaokwenda kinyume katika ”Haadiy Arwaah” ya Ibn-ul-Qayyim, ”Sharh-ut-Twahaawiyyah” ya Ibn Abiyl-´Izziy na pia Hadiyth ”Dalaalat-ul-Qur-aan wal-Athar ´laaa Ru´yati Allaahi (Ta´ala) bil-Abswaar” ya ´Abdul-´Aziyz bin Zayd ar-Ruumiy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 85-87
  • Imechapishwa: 01/11/2022