Allaah ameisifu Qur-aan Tukufu kwa sifa tukufu na nyingi. Mtunzi wa kitabu ametaja baadhi yake zifuatazo:

1 – Ya kwamba ni Kitabu cha Allaah kinachobainisha. Akimaanisha kuwa ni fasihi  juu ya zile hukumu na maelezo yaliyo ndani yake.

2 – Ya kwamba ni kamba ya Allaah imara. Akimaanisha kuwa ni agano lenye nguvu ambalo Allaah amefanya kuwa ni sababu ya kumfikia na kushinda heshima Yake.

3 – Ya kwamba ni Suurah zilizo wazi. Akimaanisha kuwa kila Suurah inatofautiana na nyingine na imara zilizohifadhiwa kutokamana na kasoro na mapungufu.

4 – Ya kwamba ni Aayah zilizobainishwa. Akimaanisha kuwa ni alama zilizo dhahiri juu ya upwekekaji wa Allaah, ukamilifu wa sifa Zake na uzuri wa kuweka kwake Shari´ah.

5 – Ya kwamba ziko Aayah za wazi na Aayah zisizokuwa wazi. Aayah zilizo wazi ni zile ambazo maana yake iko wazi na Aayah zisizokuwa wazi ni zile ambazo maana yake imejificha. Haya hayapingani na yale yaliyotangulia katika nambari 03. Kule maana yake ni kuwa imara na kuhifadhiwa kutokamana na kasoro na mapungufu. Hapa maana yake ni kuwa wazi kwa ile maana. Hapa tutapozirudisha Aayah zisizokuwa wazi kwenda katika zile zilizo wazi basi zote zinakuwa wazi.

6 – Ya kwamba ni haki isiyoweza kuingiliwa na batili katika njia yoyote:

لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيد

“Haiingiliwi na batili mbele na nyuma yake – ni Uteremsho kutoka kwa Mwenye hekima, Mwenye kuhimidiwa.”[1]

7 – Ya kwamba imetakasika kutokana na yale waliyoisifu wale wanaoikadhibisha kwamba ni mashairi:

وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنبَغِي لَهُ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُّبِينٌ

”Hatukumfunza mashairi na wala haistahiki kwake, hii si chochote isipokuwa ni ukumbusho na Qur-aan yenye kubainisha.”[2]

Wengine pia wakasema:

إِنْ هَـٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ

“Hii si chochote isipokuwa ni maneno ya mtu.”[3]

إِنْ هَـٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ

“Hii si chochote isipokuwa ni maneno ya mtu.”[4]

Hivyo Allaah akasema hali ya kumkemea aliyesema hivo:

سَأُصْلِيهِ سَقَرَ

“Nitamwingiza kwenye [Moto wa] Saqar.”[5]

8 – Ya kwamba ni miujiza; hakuna yeyote awezaye kuleta mfano wake ijapo atasaidiwa:

قُل لَّئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَن يَأْتُوا بِمِثْلِ هَـٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا

”Sema: “Lau watakusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur-aan, basi hawatoweza kuleta mfano wake japokuwa watakuwa ni wenye kusaidiana.””[6]

[1] 41:42

[2] 36:69

[3] 74:24

[4] 74:25

[5] 74:26

[6] 17:88

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 01/11/2022