48. Mfumo wa wazushi ni uleule waliokuwa nao washirikina

Nimemsikia Abu Mansuur Muhammad bin ´Abdillaah bin Hamshaad akisema: Nimemsikia Abul-Qaasim Ja´far bin Ahmad al-Muqriy ar-Raaziy akisema: ´Abdur-Rahmân bin Abiy Haatim ar-Raaziy alisomewa na huku nikisikiliza: Nimemsikia baba yangu – yaani Abu Haatim Muhammad bin Idriys al-Handhwaliy – akisema:

”Alama ya Ahl-ul-Bid´ah ni kuwatukana Ahl-ul-Athar. Alama ya mazanadiki ni kuwaita Ahl-ul-Athar Hashwiyyah kwa lengo la kutaka kuzibatilisha Athar. Alama ya Qadariyyah ni kuwaita Ahl-us-Sunnah Mujbirah. Alama ya Jahmiyyah ni kuwaita Ahl-us-Sunnah Mushabbihah. Alama ya Raafidhwah ni kuwaita Ahl-ul-Athar Naaswibah.”

Yote hayo ni ushabiki tu. Hakuna jina linalonasibiana na Ahl-us-Sunnah isipokuwa moja pekee, nalo ni Ahl-ul-Hadiyth. Isitoshe nimewaona Ahl-ul-Bid´ah wakiwaita Ahl-us-Sunnah majina yote haya bandia, wamefuata mwenendo uleule wa washirikina juu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ijapo walikuwa na mtazamo tofauti juu yake; baadhi walimwita kuwa ni mchawi, wengine wakasema kuwa ni kuhani, wengine wakasema kuwa ni mshairi, wengine wakasema kuwa ni mwendawazimu, wengine wakasema kuwa amepewa mtihani, mzushi na mwongo – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ametakasika mbali kabisa na mapungufu yote hayo. Si vyengine isipokuwa yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mteule Mtume na Nabii. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

انظُرْ كَيْفَ ضَرَبُوا لَكَ الْأَمْثَالَ فَضَلُّوا فَلَا يَسْتَطِيعُونَ سَبِيلًا

”Tazama vipi walivyokupigia mifano wakapotea, basi hawawezi kupata njia [ya kuongoka].”[1]

Vivyo hivyo wazushi; wana mtazamo tofauti juu ya Ahl-ul-Hadiyth, wabebaji wa khabari zake na wenye kunukuu Athar zake na wapokeaji wa Hadiyth zake. Baadhi wamewaita kuwa ni Hashwiyyah, wengine wakawaita kuwa ni Mushabbihah, wengine wakawaita kuwa ni Naabitah, wengine wakawaita kuwa ni Naaswibah na wengine wakawaita kuwa ni Jabriyyah. Ahl-ul-Hadiyth hawana lolote kuhusiana na mapungufu haya. Wao si jengine isipokuwa wenye kufuata Sunnah yenye kuangaza, njia ya sawa na hoja zenye kugonga na zenye nguvu. Allaah (´Azza wa Jall) amewajaalia kuweza kufuata Kitabu Chake, uteremsho na uzungumzishwaji wake na kufuata mwongozo wa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika maelezo yake aliyowaamrisha  ummah wake katika maneno na vitendo vyema na pia akawakemea katika maneno na vitendo viovu. Amewasaidia (´Azza wa Jall) kuweza kushikamana barabara na mtindo wake wa maisha na kulazimiana na Sunnah zake na vifua vyao vikakunjuka kuweza kumpenda yeye na kuwapenda maimamu wa Shari´ah yake na wanazuoni wa ummah wake. Yule mwenye kuwapenda watu basi yeye atakuwa nao siku ya Qiyaamah. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mtu atakuwa pamoja na yule anayempenda.”[2]

[1] 17:48

[2] al-Bukhaariy (6169) na Muslim (2640).

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 304-306
  • Imechapishwa: 27/12/2023