Wanapenda kwa ajili ya dini na wanachukia kwa ajili yake. Wanaepuka mijadala na mabishano juu ya Allaah. Wanawapuka Ahl-ul-Bid´ah na watu wapotevu. Wanaraddi watu wa matamanio na wajinga. Wanafuata mwongozo wake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake, ambao wao ni kama nyota; yeyote katika wao wanayemfuata, wanaongozwa. Hivo ndivo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yao. Wanawafuata Salaf kati ya maimamu wa dini na wanazuoni wa waislamu. Wanashikamana barabara na ile dini imara na haki ya wazi waliyokuwa wameishikilia.

Wanawachukia Ahl-ul-Bid´ah ambao wamezua ndani ya dini mambo yasiyokuwa ndani yake. Hawawapendi, hawajengi urafiki nao. Hawawasikilizi maneno yao na wala hawaketi nao. Hawajadili nao na wala kubishana nao. Wanaona kuwa mtu anapaswa kuyalinda masikio yake kutokana na kuzisikiza batili zao, ambazo zinapopita kwenye masikio na kukita ndani ya nyoyo, basi zinadhuru na kuleta wasiwasi na fikira mbovu. Kwa ajili yake Allaah (´Azza wa Jall) ameteremsha:

وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ وَإِمَّا يُنسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلَا تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَىٰ مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ

”Unapowaona wale wanaoziingilia na kuzishambulia Aayah Zetu, basi jitenge nao mpaka waingie kwenye mazungumzo mengineyo. Na kama shaytwaan akikusahaulisha, basi baada ya kukumbuka usikae pamoja na watu madhalimu.”[1]

[1] 6:68

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 298-299
  • Imechapishwa: 26/12/2023