Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kukisemwa: “Vipi umemjua Mola Wako?” jibu: “Kwa alama Zake na viumbe Vyake.

MAELEZO

Ukisema kuwa Allaah ndiye Mola wako au kwamba Allaah ndiye Mola wako ambaye amekulea kwa neema Zake, iko wapi dalili kwamba Allaah ndiye Mola wako ambaye amekulea kwa neema Zake? Shaykh ametaja dalili za ki-Wahy na dalili za kiakili kama itavyokuja huko mbele.

Kukisemwa… – Kwa sababu yule mwenye kudai kitu ni lazima asimamishe dalili juu ya madai yake:

Madai yasiposimamishiwa hoja

basi wenye nayo wanakuwa ni wenye kudai tu

Ni lazima kwa kila mwenye kudai kusimamisha dalili juu ya madai yake. Vinginevyo madai yake si sahihi.

Kukisemwa… – Dalili ni zepi? Jibu kwa kusema kwamba dalili ni alama na viumbe Vyake.

Maana ya Aayah kilugha ni alama ya kitu na kitu kinachojulisha jambo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Aayah za mnafiki ni tatu… “[1]

Bi maana alama.

Kwa alama Zake – Bi maana alama na viashirio vilivyojulisha juu yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Viumbe vyote hivi unavyoona vilikuwa havipo. Kisha Allaah akaviumba kwa uwezo Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Vipo viumbe vyengine vinavyojijadidi kama mfano wa mimea, watoto wachanga na vyenginevyo ambavo havikuweko kisha baadaye vikaumbwa. Nyinyi mnaviona. Ni nani ambaye ameviumba? Ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Je, vinajiumba vyenyewe? Kuna yeyote katika watu anayeviumba? Hakuna yeyote aliyeyadai haya na wala hawezi kuyadai. Amesema (Ta´ala):

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ  أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaji au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini.”[2]

Vitu hivi havikujiumba vyenyewe au havikuumbwa na mwengine katika viumbe. Kamwe kabisa hakuna yeyote aliyeumba mti, mbu wala nzi:

إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ

“Hakika wale mnaowaomba badala ya Allaah hawawezi kuumba nzi japo wakijumuika kwa hilo.”[3]

Viumbe hivi vinajulisha juu ya Muumba (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa ajili hiyo wakati mbedui mmoja wa shambani alipoulizwa ni vipi amemjua Mola Wake akajibu: “Kinyesi cha ngamia kinajulisha ngamia na athari inajulisha kitu kilichopita. Je, ulimwengu huu haujulishi kuwepo kwa Muumba?”

Ukiona athari ya mguu ardhini jambo hilo halikujulishi kuwa kuna mtu ambaye amepita juu ya ardhi hiyo? Ukiona kinyesi cha ngamia hilo halikujulishi kuwa maeneo hayo kuna ngamia au kwamba ngamia amepita juu yake? Kinyesi cha ngamia kinafahamisha kuwepo kwa ngamia na athari inajulisha kitu kilichopita sehemu hiyo.

[1] al-Bukhaariy (33) na Muslim (59).

[2] 52:35-36

[3] 22:73

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 101-104
  • Imechapishwa: 16/12/2020