Jahmiyyah wanafasiri maneno ya Allaah:

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ

“Yeye ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho.”[1]

Wanadai kuwa Allaah alikuwepo kabla ya viumbe, jambo ambalo ni kweli. Aidha wakasema kuwa atakuwa wa Mwisho baada ya kuumba kwa njia ya kwamba hakutobaki chochote, si ardhi, Pepo, Moto, malipo, adhabu, ´Arshi wala Kursiy. Wakadai kuwa hakuna chochote pamoja na Allaah na kwamba Yeye ni wa Mwisho kama Alivyokuwa. Wakawapotosha watu wengi kwa sababu ya jambo hilo.

Tukasema kuwa Allaah ametueleza kuhusu Pepo na kwamba watu wake watadumu humo milele:

يُبَشِّرُهُمْ رَبُّهُم بِرَحْمَةٍ مِّنْهُ وَرِضْوَانٍ وَجَنَّاتٍ لَّهُمْ فِيهَا نَعِيمٌ مُّقِيمٌ

”Mola wao anawabashiria rehema kutoka Kwake na radhi na mabustani yapitayo humo neema zinazodumu.”[2]

Amesema ”zenye kudumu”. Amesema tena:

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَنُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا

”Na wale walioamini na wakatenda mema, Tutawaingiza mabustani yapitayo chini yake mito, watadumu humo milele.”[3]

Amesema tena:

مَّثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ ۖ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ أُكُلُهَا دَائِمٌ وَظِلُّهَا

”Mfano wa Pepo ambayo wameahidiwa wenye  kumcha Allaah, inapita chini yake mito; makulati yake yenye kudumu na pia kivuli chake.”[4]

Allaah anapoeleza kuwa ”watadumu”, maana yake ni kwamba kamwe hazitokatika. Vilevile amesema:

وَمَا هُم مِّنْهَا بِمُخْرَجِينَ

”… nao humo hawatotolewa.”[5]

إِنَّمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا مَتَاعٌ وَإِنَّ الْآخِرَةَ هِيَ دَارُ الْقَرَارِ

”Hakika si vyenginevyo ni kwamba maisha haya ya dunia ni starehe ya kupita tu na hakika Aakhirah ndiyo nyumba ya kutulizana milele.”[6]

وَمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَهْوٌ وَلَعِبٌ ۚ وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ

”Na maisha haya ya dunia si chochote isipokuwa ni pumbao na mchezo, na hakika Nyumba ya Aakhirah bila shaka ndiyo yenye maisha ya kweli, lau wangelikuwa wanajua… !”[7]

مَّاكِثِينَ فِيهِ أَبَدًا

”Wakae humo milele.”[8]

وَأَمَّا الَّذِينَ ابْيَضَّتْ وُجُوهُهُمْ فَفِي رَحْمَةِ اللَّـهِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

”Na wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeupe, basi watakuwa katika rehema ya Allaah – wao humo ni wenye kudumu.”[9]

وَفَاكِهَةٍ كَثِيرَةٍ لَّا مَقْطُوعَةٍ وَلَا مَمْنُوعَةٍ

”… na matunda mengi hayana kikomo na wala hayakatazwi.”[10]

Mifano kama hiyo ndani ya Qur-aan ni mingi[11].

[1] 57:3

[2] 9:21

[3] 4:57

[4] 13:35

[5] 15:48

[6] 40:39

[7] 29:64

[8] 18:03

[9] 3:107

[10] 56:32-33

[11] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 168-169
  • Imechapishwa: 01/05/2024