Uombezi hauwi isipokuwa kwa masharti mawili:

Sharti ya kwanza: Allaah auidhinishe.

Sharti ya pili: Muombewaji awe ni katika watu wa Tawhiyd. Asiwe ni mshirikina. Masharti haya mawili yamechukuliwa kutoka katika Qur-aan. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?” (al-Baqarah 02:255)

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

”Na wala hawamuombei isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.” (al-Anbiyaa´ 21:27)

مَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ حَمِيمٍ وَلَا شَفِيعٍ يُطَاعُ

”Madhalimu hawatokuwa na rafiki wa dhati na wala mwombezi anayetiiwa.” (Ghaafir 40:18)

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ

”Malaika wangapi mbinguni hautowafaa kitu chochote uombezi wao  isipokuwa baada ya kuwa Allaah ametolea idhini kwa Amtakaye na kumridhia.” (an-Najm 53:26)

Hii ndio sharti ya pili. Hamridhii isipokuwa yule ambaye ni muislamu na anayemuabudu Allaah pekee. Hayuko radhi na mshirikina.

Kwa hiyo uombezi ni haki na inaombwa kutoka kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) pekee. Ama kuhusu uombezi unaoombwa kutoka kwa maiti ni uombezi batili. Allaah hakuuidhinisha. Maoni yao yatakuwa yamebatilika kwamba eti wanawaomba maiti uombezi kwa kudai kuwa uombezi ni haki. Tunasema ni haki. Lakini hata hivyo hauombwi kutoka kwa wafu. Bali unaombwa kutoka kwa Allaah. Amesema (Ta´ala):

قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا

”Sema:  “Uombezi wote ni wa Allaah.” (az-Zumar 39:44)

Uombezi ni milki ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَمْلِكُ الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ الشَّفَاعَةَ إِلَّا مَن شَهِدَ بِالْحَقِّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ

”Na wala hawana uwezo wa kumiliki uombezi wale wanaowaomba badala Yake isipokuwa aliyeshuhudia kwa haki nao wanajua.”(az-Zukhruf 43:86)

Kushuhudia kwa haki ni ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah”.

Nao wanajua bi maana wanajua maana ya neno hili na wakalifanyia kazi. Haitoshi kule kulitamka peke yake na wala mtu hajui maana yake au mtu akawa anajua lakini halitendei kazi. Haitomfaa kitu.

Jengine ni kwamba uombezi unaweza kuombwa kutoka kwa aliyehai na mbele yako. Kwa msemo mwingine unaweza kumuomba akuombee. Kwa mfano kusema: “Ewe fulani! Niombee kwa Allaah kitu fulani!” kama ambavo ´Umar alimuomba ´Abbaas aombe du´aa na kama ambavo pia watu watamuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Qiyaamah katia uwanjani.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 71-72
  • Imechapishwa: 02/09/2018