Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya shahaadah ni Kauli Yake (Ta´ala):

شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Allaah ameshuhudia kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, Malaika na wenye elimu [pia wameshuhudia], ni Mwenye kusimamisha kwa uadilifu. Hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, Mwenye nguvu kabisa asiyeshindika, Mwenye hekima.”[1]

Maana yake ni kwamba hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah. “Hapana mungu” ni kukanusha kila kinachoabudiwa badala ya Allaah, wakati “isipokuwa Allaah” ni kuthibitisha ya kwamba ´ibaadah afanyiwa Allaah pekee. Hana mshirika katika ´ibaadah Yake, kama ambavyo hana mshirika katika ufalma Wake.

Tafsiri inayoweka wazi haya, ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ إِنَّنِي بَرَاءٌ مِّمَّا تَعْبُدُونَ إِلَّا الَّذِي فَطَرَنِي فَإِنَّهُ سَيَهْدِينِ وَجَعَلَهَا كَلِمَةً بَاقِيَةً فِي عَقِبِهِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ

“Pindi Ibraahiym alipomwambia baba yake na watu wake: “Hakika mimi najitenga mbali na yale mnayoyaabudu, isipokuwa Yule aliyeniumba, basi hakika Yeye Ataniongoa! Na akalifanya neno hili kuwa ni lenye kubakia katika kizazi chake ili wapate kurejea.”[2]

Na Kauli Yake (Ta´ala):

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ ۚ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ

“Sema: “Enyi watu wa Kitabu! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu – kwamba tusiabudu yeyote isipokuwa Allaah pekee wala tusimshirikishe Yeye na chochote wala wasiwafanye baadhi yetu wengine kuwa ni waungu badala ya Allaah.” Wakikengeuka; basi semeni: “Shuhudieni kwamba sisi ni waislamu.”[3]

MAELEZO

Allaah ameambatanisha ushahidi wa wanazuoni na ushahidi wa Malaika kwa kitu ambacho ni kikubwa na kitukufu zaidi kushuhudiwa; kumshuhudia Allaah upwekekaji Wake.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hapana mungu” ni kukanusha kila kinachoabudiwa badala ya Allaah.”

Bi maana hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Huku ndio kukufuru Twaaghuut na kujitenga mbali na kila kinachoabudiwa badala Yake na kila ´ibaadah anayofanyiwa asiyekuwa Yeye.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

”… isipokuwa Allaah”.

Hapa kunathibitishwa kumuamini Allaah.

Hili ndio neno la Tawhiyd. Hapa kuna kukufuru na kuamini. Unawakufuru na kuwakanusha Twaaghuut pale unaposema:

”Hapana mungu wa haki… ”

na sambamba na hilo unamuamini Allaah pale unaposema:

”… isipokuwa Allaah.”

Amesema (Ta´ala):

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

”Basi atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, na Allaah ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa yote.”[4]

Hii ndio maana ya hapana mungu wa haki. Inakanusha shirki.

Maneno Yake (Ta´ala):

إِلَّا الَّذِي فَطَرَنِي

“… isipokuwa Yule aliyeniumba… “

Huku ni kumuamini Allaah. Inathibitishwa ´ibaadah ya Allaah baada ya kuikanusha kwa asiyekuwa Yeye. Kwa hivyo akakanusha na kuthibitisha (´alayhis-Salaam).

Maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ

“Sema: “Enyi watu wa Kitabu! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu… “

Bi maana uadilifu kati yetu sisi na nyinyi. Ni lipi neno hilo? Ni neno la Tawhiyd.

Maneno Yake (Ta´ala):

أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ

“… kwamba tusiabudu yeyote isipokuwa Allaah pekee… ”

Hii ndio maana ya shahaadah; kukanusha na kuthibitisha. Wakikubali ni sawa na wakigengeyka basi mambo ni kama alivosema Allaah:

اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ

“Shuhudieni kwamba sisi ni waislamu.”[5]

[1] 03:18

[2] 43:26-28

[3] 03:64

[4] 02:256

[5] 03:64

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 72
  • Imechapishwa: 13/02/2023