10. Maneno ya Mtume ni yenye kutangulizwa mbele ya maneno ya maimamu

Hivo ndivo walivyosema maimamu (Rahimahumu Allaah) juu ya kushikamana barabara na Hadiyth na makatazo ya kuwafuata kichwa mchunga pasi na ujuzi. Ni maneno yako wazi kabisa kwa njia ya kwamba hayakubali ubishi wala kuyapindisha. Kwa ajili hiyo yule mwenye kushikamana barabara yale yote yaliyothibiti katika Sunnah – japo wakati fulani ataenda kinyume na baadhi ya maoni ya maimamu – hazingatiwi ameyaacha madhehebu na njia yao. Bali atakuwa ni mwenye kuwafuata wote na ameshikilia kishikilio madhubuti kisichovunjika. Tofauti na hali ya ambaye ataiacha Sunnah iliyothibiti kwa sababu ya maneno ya maimamu. Atakuwa ni mwenye kuwaasi. Aidha atakuwa ameenda kinyume na maneno yao yaliyotangulia. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Basi naapa kwa Mola wako hawatoamini mpaka wakufanye wewe kuwa ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kikamilifu kabisa.”[1]

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Na atakayempinga Mtume baada ya kumbainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, Tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na uovu ulioje mahali pa kuishia!”[2]

Haafidhw Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ni wajibu kwa kila ambaye atafikiwa na maamrisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akayatambua basi awabainishie nayo Ummah, awatakie Ummah kheri na awaarishe kufuata maamrisho yake hata kama wengi katika watu wataonelea kinyume. Kwani maamrisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yana haki zaidi ya kuadhimishwa na kufuatwa kuliko maneno ya kila ambaye anaadhimishwa ambaye ameenda kinyume na maamrisho yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kimakosa. Kutokana na hili Maswahabah na wale waliokuja baada yao walimraddi kila mwenye kwenda kinyume na Sunnah Swahiyh. Huenda wakati mwingine wakawa wakali katika kuraddi[3]. Hawakufanya hivo kwa sababu wanamchukia mtu huyo. Bali mtu huyo wanampenda na kumuadhimisha, lakini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akipendwa zaidi kwao. Amri yake iko juu ya amri ya kila kiumbe. Zikigongana amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na amri ya mtu mwingine, basi amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio yenye haki zaidi ya kutangulizwa na kufuatwa. Haina maana kuwa hamuadhimishi yule ambaye kakosea hata kama atakuwa ni mwenye kusamehewa[4]. Uhakika wa mambo ni kwamba mtu huyo mwenyewe anataka kuasiwa ikiwa amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inaenda kinyume na amri yake.”[5]

Vipi watalichukulia hilo kwa ubaya ilihali wao wenyewe ndio wamewaamrisha wafuasi wao na kuwawajibishia kuyaacha maneno yao yanayokwenda kinyume na Sunnah? Bali ash-Shaafi´iy kawaamrisha wafuasi wake kuinasibisha Sunnah Swahiyh kwake ijapokuwa hakuichukua au ameonelea kinyume. Kwa ajili hiyo amesema Ibn Daqiyq-il-´Iyd (Rahimahu Allaah) wakati alipokusanya maoni ya kila madhehebu ambayo yamepingana na Hadiyth ambazo ni Swahiyh:

“Ni haramu kuyanasibisha mambo haya kwa maimamu. Ni wajibu kwa wanachuoni wenye kuwafuata kichwa mchunga kujifunza nayo na kuyajua ili wasije kuwanasibishia nayo wakawasemea uongo.”[6]

[1] 04:65

[2] 04:115

[3] Japokuwa watakuwa ni baba na wanachuoni wao. at-Twahaawiy na Abu Ya´laa wamepokea kwa cheni ya wapokezi nzuri na wapokezi waaminifu kutoka kwa Salmaan bin ´Abdillaah bin ´Umar ambaye amesema:

“Nilikuwa nimekaa pamoja na Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) msikitini wakati alipokuja mtu mmoja kutoka Shaam akamuuliza kuhusu kufanya ´Umrah pamoja na hajj. Ibn ´Umar akajibu: “Ni jambo zuri.” Ndipo mtu yule akasema: “Lakini baba yako alikuwa akikataza kufanya hivo.” Akasema: “Kuangamia ni kwako! Ikiwa baba yangu alikuwa anakataza hilo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kaliamrisha – je, utachukua maneno ya baba yangu au amri ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Akasema: “Amri ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Ibn ´Umar akasema: “Toka wende zako.” (Sharh Ma´aaniy al-Aathaar (1/372) na -Musnad (3/1317))

Ahmad (5700) amepokea mfano wake na kadhalika at-Tirmidhiy (2/82) ambaye ameisahihisha. Ibn ´Asaakir ameipokea kutoka kwa Ibn Abiy Dhi´b ambaye amesema:

“Sa´d bin Ibraahiym (mtoto wa ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf) alimhukumu mtu mmoja kwa maoni ya Rabiy´ah bin Abiy ´Abdir-Rahmaan. Nikamweleza kwamba hukumu yake inaenda kinyume na maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Matokeo yake Sa´d akasema kumwambia Rabiy´ah: “Ibn Abiy Dhi’b, ambaye kwangu ni mwaminifu, anasema kuwa hukumu yangu inatofautiana na maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Rabiy´ah akamwambia: “Umejitahidi na hukumu yake imeshapita.” Sa´d akasema: “Ajabu! Nipitishe hukumu ya Sa´d au nipitishe hukumu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Bali nafuta hukumu ya Sa´d bin Umm Sa´d na kupitisha hukumu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Akachanachana kile cheti na akahukumu kwa muqtadha wa ile hukumu.” (1/51/7)

[4] Bali ni mwenye kulipwa thawabu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atapohukumu hakimu na akajitahidi ambapo akapatia, basi ana ujira mmoja. Na atapohukumu na akajitahidi ambapo akakosea, basi ana ujira mara mbili.”  (al-Bukhaariy na Muslim)

[5] Iyqaadhw-ul-Himam, uk. 93

[6] al-Fulaaniy, uk. 99

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 48-49
  • Imechapishwa: 17/01/2019