Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Nacho si kingine ni Kitabu hiki cha Kiarabu ambacho makafiri wamesema juu yake:

لَن نُّؤْمِنَ بِهَـٰذَا الْقُرْآنِ

”Hatutoiamini Qur-aan hii.”[1]

Wengine pia wakasema:

إِنْ هَـٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ

“Hii si chochote isipokuwa ni maneno ya mtu.”[2]

Hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akasema:

سَأُصْلِيهِ سَقَرَ

“Nitamwingiza kwenye [Moto wa] Saqar.”[3]

Vilevile wakasema wengine kwamba ni mashairi. Hivyo Allaah (Ta´ala) akasema:

وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنبَغِي لَهُ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُّبِينٌ

”Hatukumfunza mashairi na wala haistahiki kwake, hii si chochote isipokuwa ni ukumbusho na Qur-aan yenye kubainisha.”[4]

Wakati Allaah alipomkanushia kuwa ni mashairi na wakati huohuo akathibitisha kuwa ni Qur-aan, hapakubaki utata kwa mtu mwenye busara ya kwamba Qur-aan ni Kitabu hichi cha Kiarabu ambacho kina maneno, herufi na Aayah, kwa sababu kisichokuwa hivyo hawezi yeyote kusema ya kwamba ni mashairi. Amesema (´Azza wa Jall):

وَإِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ

”Na ikiwa mko katika shaka yoyote kutokana na Tuliyoyateremsha juu ya mja Wetu, basi leteni Suurah moja mfano wake na waiteni mashahidi wenu pasipo na Allaah.”[5]

Haiwezekani Kwake kuwapa changamoto ya kuleta mfano wa kisichotambulika wala kueleweka. Amesema (Ta´ala):

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ ۙ قَالَ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا ائْتِ بِقُرْآنٍ غَيْرِ هَـٰذَا أَوْ بَدِّلْهُ ۚ قُلْ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أُبَدِّلَهُ مِن تِلْقَاءِ نَفْسِي

”Wanaposomewa Aayah Zetu za wazi, basi wale wasiotarajai kukutana Nasi husema: “Lete Qur-aan isiyokuwa hii au ibadilishe.” Sema: “Hainipasii mimi kuibadilisha kwa khiyari ya nafsi yangu.””[6]

Kwa hivyo Akathibitisha ya kwamba Qur-aan ni Aayah ambazo wanasomewa. Allaah (Ta´ala) amesema:

بَلْ هُوَ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ فِي صُدُورِ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ

”Bali hizo ni Aayah za wazi katika vifua vya wale waliopewa elimu.”[7]

Amesema (Ta´ala) baada ya kukiapia:

إِنَّهُ لَقُرْآنٌ كَرِيمٌ فِي كِتَابٍ مَّكْنُونٍ لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ

”Hakika hii bila shaka ni Qur-aan karimu. Katika Kitabu kilichohifadhiwa – hakuna akigusaye isipokuwa waliotakaswa.”[8]

Amesema (Ta´ala):

كهيعص

”Kaaf Haa Yaa ‘Ayyn Swaad.”[9]

حمعسق

”Haa Miym ‘Ayn Siyn Qaaaf.”[10]

Ameanza Suurah ishirini na tisa kwa herufi za kukata. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye atasoma Qur-aan na akaitamka vizuri, atapata kwa kila herufi moja thawabu kumi, na yule ambaye ataisoma kimakosa, atapata kwa kila herufi moja thawabu moja.”[11]

Hadiyth ni Swahiyh.

Amesema (´alayhis-Swalaatu was-Salaam):

“Isomeni Qur-aan kabla hawajakuja watu ambao watazisoma herufi zake vizuri pasi na kuvuka koo zao. Wanaharakia kutafuta ujira wake na wala hawaiharakii.”[12]

Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wamesema:

“Kuisoma Qur-aan vizuri kunapendekezwa zaidi kwetu kuliko kuhifadhi baadhi ya herufi zake.”[13]

´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mwenye kukufuru herufi moja, basi huyo kakufuru Qur-aan nzima.”[14]

Waislamu wote wamekubaliana juu ya idadi ya Suurah za Qur-aan, Aayah zake, maneno yake na herufi zake. Hakuna tofauti kati ya waislamu ya kwamba mwenye kukanusha kutoka katika Qur-aan, sawa iwe ni Suurah moja, Aayat moja, neno moja au herufi waliyoafikiana kwayo, ya kwamba ni kafiri. Katika hili kuna hoja madhubuti ya kwamba [Qur-aan ni] herufi.

MAELEZO

Qur-aan ni herufi na maneno. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ametaja dalili nane juu ya hilo:

1 – Makafiri walisema kuwa ni mashairi. Hakiwezi kusifiwa hivo isipokuwa kile ambacho ni herufi na maneno.

2 – Allaah amewapa changamoto wale wanaoikadhibisha walete mfano wake. Kama ingelikuwa sio herufi na maneno basi changamoto hiyo ingelikuwa si yenye kukubaliwa. Mtu hawezi kupewa changamoto isipokuwa kwa kitu kinachotambulika na kufahamika.

3 – Allaah ameeleza kwamba wanasomewa Qur-aan:

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ ۙ قَالَ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا ائْتِ بِقُرْآنٍ غَيْرِ هَـٰذَا أَوْ بَدِّلْهُ ۚ قُلْ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أُبَدِّلَهُ مِن تِلْقَاءِ نَفْسِي

”Wanaposomewa Aayah Zetu za wazi, basi wale wasiotarajai kukutana Nasi husema: “Lete Qur-aan isiyokuwa hii au ibadilishe.” Sema: “Hainipasii mimi kuibadilisha kwa khiyari ya nafsi yangu.””

Hakisomwi isipokuwa ambacho ni herufi na maneno.

4 – Allaah amekhabarisha kuwa imehifadhiwa ndani ya vifua vya wanazuoni na imeandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa:

بَلْ هُوَ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ فِي صُدُورِ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ

”Bali hizo ni Aayah za wazi katika vifua vya wale waliopewa elimu.”

إِنَّهُ لَقُرْآنٌ كَرِيمٌ فِي كِتَابٍ مَّكْنُونٍ لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ

”Hakika hii bila shaka ni Qur-aan karimu. Katika Kitabu kilichohifadhiwa – hakuna akigusaye isipokuwa waliotakaswa.”

Hakihifadhiwi na kuandikwa isipokuwa kile ambacho ni herufi na maneno.

5 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye atasoma Qur-aan na akaitamka vizuri, atapata kwa kila herufi moja thawabu kumi, na yule ambaye ataisoma kimakosa, atapata kwa kila herufi moja thawabu moja.”

Ameisahihisha mtunzi wa kitabu na hakuiegemeza na wala sijampata ambaye ameipokea.

6 – Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wamesema:

“Kuisoma Qur-aan vizuri kunapendekezwa zaidi kwetu kuliko kuhifadhi baadhi ya herufi zake.”

7 – ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mwenye kukufuru herufi moja, basi huyo kakufuru Qur-aan nzima.”

8 – Waislamu wameafikiana – kama alivyonukuu mtunzi – juu ya kwamba yeyote atakayepinga Suurah, Aayah, neno au herufi hata moja ambayo kuna maafikiano juu yake, basi ni kafiri[15].

Idadi ya Suurah za Qur-aan ni 114. Katika hizo kuna Suurah 29 ambazo zimeanza kwa herufi za mkato.

[1] 34: 31

[2] 74:25

[3] 74:26

[4] 36:69

[5] 02: 23

[6] 10:15

[7] 29:49

[8] 56:77-79

[9] 19:01

[10] 42:01-02

[11] as-Suyuutwiy katika ”al-Haawiy” (1/564) na at-Twabaraaniy katika ”al-Kabiyr” (6021) na pia “al-Awsatw”.

Tanbihi muhimu! Hadiyth hii ni dhaifu. Imaam al-Haythamiy (Rahimahu Allaah) amesema: “Kumekuja Nahshal na ni mwenye kuachwa.”Nahshal ni Ibn Sa´iyd bin Wardaan al-Wardaaniy na Imaam Ishaaq bin Raahawayh (Rahimahu Allaah) amesema kuwa ni mwongo.

[12] Ahmad (5/338), Abu Daawuud (831) na Ibn Hibbaan (1876). Katika Hadiyth hii kunakuja udhaifu kwa sababu ya Wafaa´ bin Shariyh ambaye ametajwa katika cheni ya wapokezi. Hata hivyo Hadiyth hii imepewa nguvu na Hadiyth zifuatazo, kwa mfano Hadiyth iliyopokelewa na Jaabiyr bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anh) ambayo imekuja pia kwa Ahmad (3/397) na Abu Daawuud (830). Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh ambayo Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) ameitaja katika “as-Silsilah as-Swahiyhah” (259).

[13] Ibn Qudaamah katika ”al-Burhaan”, uk. 44, na Ibn Anbaariy katika ”al-Waqf al-Ibtidaa´” (1/20).

[14] Ibn Abiy Shaybah (1/102) na (10/513) na Ibn Jariyr katika ”Jaamiy´-ul-Bayaam ´an Ta´wiyl Aayat-il-Qur-aan” (56).

[15] al-Burhaan, uk. 49-51 ya Ibn Qudaamah ambaye amenakili maafikiano juu ya hilo na mambo mengi yanayohusiana na jambo hilo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 79-84
  • Imechapishwa: 31/10/2022