45. Qur-aan ni maneno ya Allaah, yaliyoteremshwa na hayakuumbwa

Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Miongoni mwa maneno ya Allaah (Subhaanah) ni Qur-aan Tukufu. Nacho ni Kitabu cha Allaah chenye kubainisha, kamba Yake imara na Njia Yake iliyonyooka na ni Uteremsho kutoka kwa Mola wa walimwengu. Umeteremsha Roho Mwaminifu kwenye moyo wa kiongozi wa Mitume kwa lugha ya Kiarabu iliyo wazi. Imeteremshwa na wala haikuumbwa, imeanza kutoka Kwake na Kwake ndiko itarudi. Ni Suurah zilizo wazi na Aayah zilizobainishwa, herufi na maneno. Yule mwenye kuisoma na akaitamka ipasavyo anapata kwa kila herufi moja thawabu kumi. Yana mwanzo na mwisho, sehemu na vipande. Inasomwa kwa midomo, imehifadhi kwenye vifua, inasikizwa kwa masikio na kuandikwa katika misahafu. Ndani yake kuna [Aayah za] zilizo wazi na sizizokuwa wazi, zinazofuta na zilizofutwa, ambazo ni maalum na zilizoenea, za maamrisho na za makatazo:

لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِتَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيد

“Haiingiliwi na batili mbele na nyuma yake – ni Uteremsho kutoka kwa Mwenye hekima, Mwenye kuhimidiwa.”[1]

قُل لَّئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَن يَأْتُوا بِمِثْلِ هَـٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا

”Sema: “Lau watakusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur-aan, basi hawatoweza kuleta mfano wake japokuwa watakuwa ni wenye kusaidiana.””[2]

MAELEZO

Qur-aan Tukufu ni maneno ya Allaah (Ta´ala) iliyoteremshwa na haikuumbwa. Kwake ndiko imeanza na Kwake ndiko itarudi. Kwa hiyo ni maneno ya Allaah. Ni mamoja herufi na maana yake. Dalili kwamba ni maneno ya Allaah ni maneno Yake (Ta´ala):

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ

“Endapo mmoja katika washirikina atakuomba umlinde, basi mlinde mpaka aweze kusikia maneno ya Allaah.”[3]

Bi maana Qur-aan.

Dalili ya kwamba ni yenye kuteremshwa ni maneno Yake (Ta´ala):

تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَى عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا

“Amebarikika Yule ambaye ameteremsha Pambanuzi kwa mja Wake ili awe ni muonyaji kwa walimwengu.”[4]

Dalili ya kwamba haikuumbwa ni maneno Yake (Ta´ala):

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ

”Tanabahi! Uumbaji ni Wake pekee na kupitisha amri.”[5]

Ametofautisha amri na uumbaji. Qur-aan ni katika amri Zake. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِّنْ أَمْرِنَا

“Na hivyo ndivyo tulivyokuletea Roho katika amri Yetu.”[6]

ذَٰلِكَ أَمْرُ اللَّـهِ أَنزَلَهُ إِلَيْكُمْ

“Hiyo ni amri ya Allaah amekuteremshieni.”[7]

Isitoshe maneno ya Allaah ni sifa miongoni mwa sifa Zake na sifa Zake hazikuumbwa.

Dalili kwamba Kwake ndiko imeanza ni kuwa Allaah ameyaegemeza maneno Kwake. Hayaegemezwi maneno isipokuwa kwa Yule aliyeanza kuyasema mara ya kwanza.

Dalili kwamba Kwake ndiko itarudi ni kuwa imepokelewa katika baadhi ya mapokezi kwamba:

“Itapofika zama za mwisho itaondolewa kutoka ndani ya misahafu na kwenye vifua.”[8]

[1] 41:42

[2] 17:88

[3] 09:06

[4] 25:01

[5] 07:54

[6] 42:53

[7] 65:05

[8] Ibn Maajah (4049) na al-Haakim (04/473) ambaye amesema:

”Ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za Muslim.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye. al-Albaaniy amesema katika “as-Swahiyhah (87)”:

“Mambo ni kama alivosema.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 76-79
  • Imechapishwa: 31/10/2022