46. Ni ipi hukumu ya kuangalia mechi za mpira na nyinginezo?

Swali 46: Ni ipi hukumu ya kuangalia mechi za mpira na nyinginezo?

Jibu: Wakati wa mtu ni kitu chenye thamani[1]. Asiupoteze katika kuangalia mechi za mpira. Mechi zinamshughulisha kutokana na utajo wa Allaah[2]. Kuna  khatari vilevile pengine zikamvuta na yeye mwenyewe akawa mchezaji katika siku zijazo. Hivyo akatoka katika matendo muhimu na kazi zenye manufaa na kwenda katika matendo yasiyokuwa na faida yoyote.

[1] Inampasa muislamu apupie wakati wake na autumie wakati na umri wake katika kumtaja Allaah, kumtii Allaah na kuitafuta elimu yenye manufaa. Hebu tujikumbushe Hadiyth ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa mteule (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia bwana mmoja wakati alipokuwa akimpa mawaidha:

”Tumia fursa ya matano kabla ya matano: ujana wako kabla ya uzee wako, uzima wako kabla ya ugonjwa wako, utajiri wako kabla ya ufukara wako, faragha yako kabla ya shughuli yako, uhai wako kabla ya kifo chako.” (Ameipokea al-Haakim (4/306) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye)

[2] Mtu ataulizwa juu ya kila kitu cha kheri na shari alichokifanya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Haitovuka miguu ya mja siku ya Qiyaamah mpaka aulizwe juu ya mambo manne: umri wake aliuteketeza katika mambo gani, ujana wake aliutumia vipi, mali yake aliipata kivipi na akaitumia wapi na elimu yake aliifanyia nini.”  (Ameipokea al-Bayhaqiy kupitia kwa Mu´aadh bin Jabal na at-Tirmidhiy (2417) kupitia kwa Abu Barzah al-Aslamiy kwa tamko lisemalo ”na mwili wake” badala ya ”ujana wake”. Tazama ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (1/126))

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 131-132
  • Imechapishwa: 03/03/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy