46. Ili mswaliji ahesabike amewahi Rak´ah ni lazima awahi kuleta Tasbiyh?

Swali 46: Ni kipi kilichosuniwa kwa ambaye amekuja amechelewa akimkuta imamu yuko katika Rukuu´? Hukumu ya kuwahi Rak´ah ni sharti awahi kusema:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola wangu aliyetukuka.”

kabla ya imamu kuinuka?

Jibu: Maamuma akimuwahi imamu hali ya kurukuu Rak´ah hiyo imesihi ijapo hakuwahi kuleta Tasbiyh isipokuwa baada ya imamu kuinuka. Hayo ni kutokana na kuenea kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayewahi Rak´ah ya swalah, basi ameiwahi swalah.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Ni jambo linalotambulika kuwa Rak´ah inawahiwa kwa kuwahi Rukuu´. Hilo ni kutokana na yale aliyopokea al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Bakrah ath-Thaqafiy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Ya kwamba siku moja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkuta amerukuu ambapo na yeye akarukuu nje ya safu. Kisha akajiunga ndani ya safu. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotoa salamu akamwambia:

“Allaah akuzidishie pupa na usirudie.”

Hakumwamrisha kulipa Rak´ah nyingine. Alichomkataza ni kujiunga na swalah nje ya safu. Kwa hivyo ni lazima kwa ambaye amekuja kuchelewa asifanye haraka ya Rukuu´ mpaka kwanza afike katika safu.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 53-54
  • Imechapishwa: 01/09/2022