Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

”Wewe pekee ndiye tunakuabudu… ”[1]

Yaani hatumuabudu mwengine yeyote badala Yako. Hii ni ahadi iliopo baina ya mja na Mola Wake ya kwamba hatomuabudu mwengine asiyekuwa Yeye.

وإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“… na Wewe pekee ndiye tunakutaka msaada.”[2]

Yaani ni ahadi iliopo baina ya mja na Mola Wake kwamba hatoomba msaada kwa mwengine asiyekuwa Yeye.

MAELEZO

Kutangulizwa:

إِيَّاكَ

”Wewe pekee…”

kunaleta maana ya ufupikaji na umaalum. Maana yake ni kwamba, ee Allaah, tunakukhusisha Wewe pekee kwa ´ibaadah na tunakuabudu Wewe na wala hatumwabudu mwengine asiyekuwa Wewe.

Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah imekusanya kukanusha na kuthibitisha. Unakanusha pale unaposema:

“Hapana mungu wa haki.”

Hapa  wanakanushwa waungu wote wa wongo na kujitenga mbali na kila kinachoabudiwa kisichokuwa Allaah.

Unathibitisha pale unaposema:

“… isipokuwa Allaah.”

Hapa kunathibitishwa ´ibaadah kufanyiwa Allaah pekee na kumwamini Yeye.

Hakuna Tawhiyd isipokuwa kwa mambo mawili:

1 – Kukanusha.

2 – Kuthibitisha.

Kumkanushia ´ibaadah asiyekuwa Allaah na sambamba na hilo kumthibitishia nayo Allaah. Aidha kuwakanusha waungu wote wa wongo na kumwamini Allaah. Amesema (Ta´ala):

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٌٰ

”Basi atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti.”[3]

Maneno yake:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ

”Wewe pekee ndiye tunakuabudu… ”

Tunakuabudu Wewe na hatumwabudu mwengine asiyekuwa Wewe. “Tunakuabudu Wewe”, hapa kuna kuthibitisha. “Hatumwabudu mwengine asiyekuwa Wewe”, hapa kuna kukanusha. Kwa hiyo maana ya:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ

”Wewe pekee ndiye tunakuabudu… ”

ikawa ndio maana ya “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.”

Maneno yake:

“Hii ni ahadi iliopo baina ya mja na Mola Wake ya kwamba hatomuabudu mwengine asiyekuwa Yeye.”

Hii ni ahadi na kujilazimisha. Kwa msemo mwingine ni kwamba umejilazimisha na kumwahidi Mola wako ya kwamba hutomwabudu mwengine asiyekuwa Yeye.

Maneno yake:

وإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“… na Wewe pekee ndiye tunakutaka msaada.”

Tunakuomba msaada, ee Allaah, na hatumwombi msaada mwengine asiyekuwa Wewe.

Maneno yake:

“Ahadi iliopo baina ya mja na Mola Wake kwamba hatoomba msaada kwa mwengine asiyekuwa Yeye.”

Hii ni ahadi na kujilazimisha. Kwa msemo mwingine ni kwamba umejilazimisha na kumwahidi Mola wako ya kwamba hutomwomba msaada mwengine asiyekuwa Yeye. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Allaah (Ta´ala) amesema: “Nimeigawanya swalah kati Yangu Mimi na mja wangu mafungu mawili na mja Wangu atapata kile anachoomba… Mja akisema:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“Wewe pekee ndiye tunakuabudu na Wewe pekee ndiye tunakuomba msaada.”[4]

Husema:

“Hili ni kati Yangu mimi na mja Wangu na mja wangu atapata kile alichoomba… “[5]

[1] 01:05

[2] 01:05

[3] 02:256

[4] 01:05

[5] Muslim (395).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 74-76
  • Imechapishwa: 16/06/2022