45. Maoni yaliyochaguliwa na Ibn ´Uthaymiyn kuhusu kupangusa juu ya kitu kinachofunika mguu

بسم الله الرحمن الرحيم

و الصلاة و السلام على نبينا محمد و على آله و أصحابه أجمعين

Masuala haya yanahusu kupangusa juu ya soksi za ngozi. Nimefupizika na yale maoni niliyoona kuwa ni ya sawa kwa mujibu wa dalili za Shai´ah. Namwomba Allaah (Ta´ala) kazi hii iwe takasifu kwa ajili Yake na yenye kuafikiana na Shari´ah ya Allaah.

1 – Wanazuoni (Rahimahumu Allaah) wametofautiana kuhusu kufaa kupangusa juu ya soksi za ngozi zilizo na matundu. Maoni sahihi ni kwamba inafaa muda wa kuwa kitu hicho kinachofunika mguu bado zinaitwa ”soksi za ngozi”. Haya ndio maoni ya Ibn-ul-Mundhir ambayo ameyanukuu kutoka kwa ath-Thawriy, Ishaaq, Yaziyd bin Haaruun na Abu Thawr. Haya ndio maoni pia ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah muda wa kuwa bado kitu hicho kinachofunika mguu kinaitwa ”soksi za ngozi” na mtu anaweza kutembea juu yake.

2 – Kwa mujibu wa maoni sahihi ni kwamba inafaa kupangusa juu ya soksi nyembamba. an-Nawawiy amesema:

“Wenzetu wamenukuu kutoka kwa ´Umar na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambao wamejuzisha kupangusa juu ya soksi za ngozi hata kama zitakuwa nyembamba. Pia wamenukuu hayohayo kutoka kwa Abu Yuusuf, Muhammad, Ishaaq na Daawuud.”[1]

Amesema tena:

“Maoni sahihi ni yale yaliyosemwa na Abut-Twayyib, al-Qaffaal na jopo la wahakiki wengine, kwamba inafaa muda wa kuwa kuna uwezekano wa kutembea juu yake pasi na kujali zilivyo. Vinginevyo haitofaa.

3 – Muda wa kupangusa ni mchana mmoja na usiku wake kwa ambaye ni mwenyeji na michana mitatu na nyusiku zake kwa ambaye ni msafiri. Muda wa kupangusa unaanza kuhesabiwa kuanzia pale mara ya kwanza atapangusa baada ya kuchenguka kwa wudhuu´. Haya ndio maoni sahihi zaidi na ni moja ya upokezi wa Ahmad. Haya ndio maoni alionayo al-Awzaa´iy, Abu Thawr na Ibn-ul-Mundhir ambaye amenukuu mfano wake kutoka kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). an-Nawawiy amesema:

“Ndio maoni yenye dalili yenye nguvu.”

4 – Mtu akifuta akiwa ndani ya mji wake kisha akafunga safari kabla ya kuchengukwa na wudhuu´,  basi atapangusa kama msafiri.

5 – Mtu akipangusa soksi zake za ngozi safarini kisha akarudi katika mji wake kabla ya kuchengukwa na wudhuu´, basi atapangusa kama mwenyeji.

6 – Mtu akipangusa soksi za ngozi katika mji wake, akachengukwa na wudhuu´ kisha akasafiri kabla ya kupangusa, basi atapangusa kama msafiri.

7 –  Mtu akipangusa katika safari, akachengukwa na wudhuu´ kisha akarudi katika mji wake kabla ya kupangusa, basi atapangusa kama mkazi.

8 – Mtu akipangusa soksi za ngozi katika mji wake, akachengukwa na wudhuu´ halafu akasafiri kabla ya kumalizika ule muda wa kupangusa, basi atapangusa kama msafiri. Haya ndio maoni sahihi zaidi. Haya ndio maoni ya Abu Haniyfah na upokezi ambao Ahmad alirejea kwao. Imekuja katika “al-Faaiq” ifuatavyo:

“Haya ndio maneno ya nyuma na yaliyochaguliwa.”

 Muda wa kupangusa ukimalizika kabla ya yeye kusafiri,  basi atalazimika kuosha miguu yake wakati wa kutawadha.

9 –  Mtu akipangusa safarini, akachengukwa na wudhuu´, akapangusa soksi zake za ngozi kisha akarudi katika mji wake, basi atapangusa kama mkazi ikiwa kumebaki kitu katika muda wake. Vinginevyo atazivua. Imekuja katika “al-Mughniy”:

“Hatujui tofauti yoyote kutoka kwa wanazuoni juu ya hilo.”

10 – Mtu akivaa soksi za kawaida au soksi za ngozi kisha akavaa juu yake pea nyingine kabla ya kuchengukwa na wudhuu´, basi atapangusa yoyote anayotaka.

11 – Mtu akivaa soksi za kawaida au soksi za ngozi, akachengukwa na wudhuu´ kisha akavaa juu yake pea nyingine kabla ya kutawadha, basi atapangusa ile pea ya chini.

12 – Mtu akivaa soksi za kawaida au soksi za ngozi, akachengukwa na wudhuu´, akapangusa juu yake kisha akavaa juu yake pea nyingine, basi atapangusa ile pea ya juu. Haya ndio maoni sahihi zaidi. Imekuja katika “al-Furuu´” ifuatavyo:

“Hata hivyo yale maoni yanayojuzisha yana mtazamo fulani, kama anavoonelea Maalik.”

an-Nawawiy amesema:

“Haya ndio maoni yenye nguvu na yanayochaguliwa kwa sababu amezivaa akiwa na twahara. Fikira yao kwamba ni twahara pungufu ni jambo la kimakosa.”

Kujengea juu ya hayo muda wa kupangusa unaanza kuanzia katika ule mpanguso wa kwanza.

13 – Mtu akivaa pea juu ya pea nyingine, akapangusa ile pea ya juu kisha akaivua, je, ule muda uliobaki anaweza kupangusa ile pea ya chini? Sijaona mtu ambaye amesema hivo waziwazi, lakini an-Nawawiy ametaja kwamba Abul-´Abbaas bin Surayj ametaja maana tatu juu ya hilo ambapo akivaa gaita juu ya soksi za ngozi ni kwamba ni kama soksi za ngozi moja; ile ya juu ni kama sehemu ya juu na ile ya chini ni kama seemu ya chini. Kutokana na hili inafaa kupangusa katika ile pea ya chini midhali bado upo muda wa kupangusa kwa ile pea ya juu kama ambavo kunafutwa sehemu ya ndani ya soksi za ngozi ikiwa ile sehemu yake ya nje imepasuka.

14 – Twahara yake haichenguki pale ambapo atavua soksi zake za ngozi au za kawaida baada ya kuzipangusa. Mtu huyu ataswali swalah atakazo mpaka pale atapochengukwa na wudhuu´. Haya ndio maoni sahihi zaidi. Ibn-ul-Mundhir ameyanukuu kutoka kwa kikosi katika wanafunzi wa Maswahabah. Maoni haya yamechaguliwa na Ibn Hazm na akasema ndio maoni ya wengi katika Salaf. an-Nawawiy amesema:

“Ndio maoni yenye kuchaguliwa na yenye nguvu.”

Ndio maoni yaliyochaguliwa pia na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah.

15 – Twahara haichenguki kwa kumalizika ule muda wa kupangusa. Mtu huyu ataswali swalah atakazo mpaka pale atapochengukwa na wudhuu´. Haya ndio maoni sahihi zaidi na pia yamechaguliwa na wale wenye kuona kwamba wudhuu´ hauchenguki katika suala la kabla yake. Ibn Hazm amesema:

“Haya ndio maoni pekee yanayojuzu.”

Ibn Hazm amesema tena:

“Akipangusa dakika moja kabla ya kumalizika kwa muda, basi inafaa kwake kuswali kwa hali hiyo midhali wudhuu´ wake haujachenguka.”[2]

Na Allaah ndiye mjuzi zaidi. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake na wale watakaowafuata mpaka siku ya Malipo.

Imeandikwa tarehe 07 Rabiy´ ath-Thaniy 1411 na himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] al-Majmuu´ (1/484).

[2] al-Muhallaa (2/95).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/191-194)
  • Imechapishwa: 11/05/2021