Msingi, ambao ndio hoja yetu, ni kufuata yale yaliyozungumzwa na Qur-aan. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho.”[1]

Tukilirudisha jambo katika yale ambayo Allaah amemtumiliza na kumteremshia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi tutaona kuwa amefanya imani ni kule kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Karibu miaka kumi na tatu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwalingania watu Makkah katika shahaadah hii peke yake. Kipindi hicho shahaadah pekee yake ndio ambayo ilikuwa imefaradhishwa juu ya waja. Yule mwenye kuikubali ndiye ambaye alikuwa ni muumini na hakuitwa kitu kingine. Hawakuwa wakilazimishwa kutoa zakaah, kufunga wala kitu kingine cha dini. Wanazuoni wanaona kuwa kipindi hicho ilikuwa ni kwa sababu ya kuwafanyia wepesi watu kwani ni punde tu wametoka katika ukafiri na uzembeaji na hivyo faradhi nyenginezo zingewashtua na kuwakimbiza. Kwa ajili hiyo kule kukiri kwa mdomo peke yake ndio kukafanywa kuwa ni jambo lililofaradhishwa kwa watu kipindi hicho. Hivo ndivo hali ilivyokuwa Makkah kipindi chote na takriban miezi kumi baada ya kuhajiri Madiynah.

[1] 04:59

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 12/05/2021
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy